UONGOZI wa Shule ya Sekondari Kilimani,umepokea msaada wa mifuko 50 ya saruji yenye thamani ya 1,000,000 kutoka kwa Mbunge wa Ilemela (CCM),Dk.Angelline Mabula,ili kuboresha miundombinu ya madarasa kutokana na uchakavu wa sakafu.
Saruji hiyo ilikabidhiwa juzi na Katibu wa Mbunge huyo,Kazungu Idebe kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kilimani Sekondari,Juma Mongu,kwa niaba ya Dk. Mabula.
Alisema saruji hiyo mifuko 50 itasaidia kuondoa tatizo la uchakavu wa sakafu za vyumba vitano vya madarasa ya shule hiyo na kuboresha mazingira ya ufundishaji na kujifunzia.
Idebe alisema uwekezaji ama mbegu ya vitabu vya kujifunzia na kufundishia iliyopandwa na Dk. Mabula kwenye shule hiyo, matunda yake yameanza kuonekana na kuwahimiza wanafunzi kuongeza bidii na nidhamu kwenye masomo kwani uboreshaji wa miundombinu unaofanywa na wazazi ni kwa maslahi yao.
“Penye nia inawezekana watu wakitubutu,niwapongeze kwa kujenga hosteli ya wasichana,hii ni kumlinda mtoto wa kike na changamoto za mtaan ili atapate fursa ya kujisomea na hata hizo Division One hapa hazikuja bahati mbaya.Pia uboreshaji wa miundombinu na taaluma utaifanya Kilimani sekondari kuwa shule bora ya mfano,”alisema Kazungu.
Aliongeza; “Mlikuwa na maombi mawili ya saruji mifuko 50 hilo nimemaliza,la vitendea kazi (kompyuta,mashine nukushi ya kudurufu maandishi na printa) niachieni nitalifanyia kazi maana hayo ni majukumu yangu kupitia Kauli mbiu ya Hapa Zege Halilali,muhimu tuendelee kushikamana ili ya kukuza na kuongeza ufaulu wa watoto wetu,”alisema kwa niaba ya Dk. Mabula.
Awali akisoma risala Mkuu wa Shule ya Kilimani,Majaliwa Gerana,alisema Mbunge huyo wa Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi,amekuwa mdau mkubwa wa elimu jimboni humo,akihakikisha anapunguza changamoto za elimu kwenye shule za sekondari na msingi.
Alimshukuru Dk. Mabula kwa namna anavyoshiriki kwenye maendeleo ya miundombinu na taaluma ya Kilimani ambapo awali alitoa matofali 6,000 ya ujenzi wa maboma matatu ya madarasa na uzio wa hosteli ya wasichana,vitabu 240 vya hesabu huku Halmashauri ya Ilemela ikichangia matofali 2,000 pamoja na kukamilisha maboma hayo kwa kuyaezeka.
“Kwa niaba ya jumuiya ya Shule ya Kilimani Sekondari tunakushukuru kwa mifuko hii 50 ya saruji uliyotupatia,itawezesha vyumba vitano vya madarasa kuwekewa sakafu,hii itachochea uboreshaji mazingira ya kujifunzia na kufundishia,kuongeza ufaulu wa wanafunzi wetu na kuinua ari ya kupenda shule.Hakika wewe ni mdau namba moja wa elimu Ilemela,”alisema.
Gerana alisema licha ya mafanikio ya kitaaluma kwa miaka mitatu,bado wakabiliwa na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo,viti na meza za walimu na wanafunzi,vitendea kazi kama kompyuta,mashine nukushi na printa.
Alisema changamoto nyingine ni upatikanaji duni wa huduma ya maji unaosababisha usumbufu kwa wanafunzi na kuvuruga ratiba za kitaaluma (masomo),ambapo maji yanapokatika watoto hulazimika kwenda kuyatafuta umbali mrefu na kumwomba Mbunge huyo wa Ilemela kuona namna ya kuwasaidia kuzitatua.
Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo,Juma Mongu,alisema wanatafuta kujenga ufaulu wa daraja la kwanza,ili kufikia azma hiyo wanajiandaa kujenga hosteli ya wavulana na wasichana lakini wanatatizwa na mwingiliano wa jamii kuvamia maeneo ya shule na kujenga makazi ya kudumu.