Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Lindi
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda leo tarehe 5 Juni 2021 ameshiriki na kushuhudia Chama Kikuu ha Ushirika Lindi Mwambao katika kijiji cha Luhokwe Kata ya Mnonela Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi kikifanya mnada wa Pili (2) wa zao la Ufuta kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mafanikio makubwa.
Katika mnada huo wa pili Waziri Mkenda ameshuhudia wakulima wakikubali kuuza Jumla ya Kilogramu 3,728,417 za Ufuta ambapo Kampuni 17 zimeshiriki huku kampuni saba ndizo zilizoshinda ununuzi huo
Jumla ya Wakulima 417 wamekubali kuuza ufuta wao kwa bei ya juu ya Tsh 2,371 kwa kilo moja na bei ya chini ya Tsh 2,253 kwa kilo moja. Mahitaji ya wanunuzi yalikuwa ni jumla ya kilo 10,783,417.
Katika ghala la BUCO jumla ya Kilogramu 1,533,242 zimeuzwa kupitia kampuni ya Dizygotic ikinunua Tani 90 kwa Tsh 2,339, Kampuni ya Export imenunua Tani 400 kwa Tsh 2,315, Kampuni ya Dizygotic Tani 120 kwa Tsh 2,303, Kampuni ya Afrisian Tani 200 kwa Tsh 2,292, Kampuni ya S.M Holding Tani 115 Tsh kwa 2,270, Kampuni ya H.S Impex Tani 500 kwa Tsh 2,255 na Kampuni ya RBST Tani 108 kwa Tsh 2,253.
Katika ghala la MTAMA jumla ya Kilogramu 782,700 zimeuzwa kwa Kampuni ya Export iliyonunua Tani 400 kwa Tsh 2,261 na Kampuni ya RBST ikinunua Tani 383 kwa Tsh 2,253. Vilevile katika Ghala la NANGURUKURU zimeuzwa jumla Kilogramu 1,412,475 ambapo Kampuni ya Export ikinunua Tani 500 kwa Tsh 2,371 na Kampuni ya RBST ikinunua Tani 912 kwa Tsh 2253.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mnada huo Waziri Mkenda amewapongeza wakulima hao kukubali kwa kauli moja kuuza Ufuta huku akisisitiza umuhimu wa mfumo wa Stakabadhi ghalani ambao kwa kiasi kikubwa umewanufaisha wakulima katika mazao yote ambayo yanaingia kwenye mfumo huo ikiwemo usimamizi thabiti wa Ushirika.
Amesema kuwa Stakabadhi ghalani inawezekana na itasaidia katika maeneo mengine kufanya mnada mzuri ambapo ameutaja mkoa wa Lindi kuwa mkoa wa pili kwa uzalishaji wa Ufuta nchini baada ya mkoa wa Morogoro hivyo serikali itaendelea kuweka mkazo na msisitizo Zaidi katika kuhakikisha Tija na masoko vinaimarishwa.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa zipo changamoto zinazoikabili sekta ya Ushirika ambazo zitatafutiwa ufumbuzi wa haraka lakini sio kuuondoa mfumo huo ambao umekuwa na motisha kwa wakulima wa mazao mbalimbali nchini.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Mtama Mhe Nape Nnauye amesema kuwa mfumo wa Ushirika na Stakabadhi ghalani umekuwa mkombozi kwa wakulima katika mkoa wa Lindi kwani umewahakikishia wananchi bei nzuri ya mazao yao ikiwemo Korosho.
Naye Mrajisi kuu wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt Benson Ndiege amesema kuwa changamoto zote zinazoikabili sekta ya Ushirika zitaendelea kutatuliwa ili kuiimarisha sekta hiyo.