Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akipokea ngao ya ushindi wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii katika maonesho ya pili ya Elimu na mafunzo ya ufundi kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole Sadick Rajab katika Ofisi za Wizara, Jijini Dodoma.
Mratibu wa maonesho ya pili ya elimu na mafunzo ya ufundi na Mkufunzi wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Muhdin Galiatano akieleza jambo wakati wa kumkabidhi Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, ngao ya ushindi wa kwanza katika maonesho hayo yaliyofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike akieleza jambo mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, wakati wa makabidhiano ya ngao ya ushindi wa kwanza katika maonesho ya pili ya elimu ya ufundi yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dodoma.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WAMJW)
*********************************
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema njia pekee ya kukabiliana na ukosefu wa ajira ni kuwaandaa wahitimu mumkakati ili waweze kuajirika, kujiajiri na kuajiri wengine.
Dkt. Jingu amesema hayo Jijini Dodoma wakati akipokea ngao ya ushindi wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii Ufundi katika maonesho ya pili ya Elimu ya mafunzo na ufundi yaliyoandaliwa na Baraza la Elimu ya ufundi (NACTE).
Dkt. Jingu amesema ushindi huo umetokana na jitihada za kuimarisha taaluma inayotolewa kwa wahitimu ikilenga kutatua changamoto za maendeleo katika Jamii husika.
“Kwanza tumeweza kufanya mapinduzi kwenye elimu tunayotoa katika vyuo vyetu. Vyuo vyetu vya maendeleo ya jamii havijikiti tu kutoa shahada au vyeti kwa ajili ya kutundika ukutani au kuzunguka na bahasha, sasa hivi tunawafundisha wanafunzi wetu kujiajiri na kuajirika na kuajiri wengine. Ndiyo maana wahitimu wetu hawazunguki sana mtaani kutafuta ajira, wengi wao wanapambana kujiajiri kwa sababu wamejengewa ujuzi na maarifa ya kujiajiri” alisema Dkt. Jingu.
Ameongeza kuwa
dhana tatu zilizoanzishwa na vyuo hivyo ambazo ni ubunifu, uanagenzi na ushirikishaji jamii ni muhimu sana katika kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiari na kuajirika hivyo ziendelee kutumika na kuimarishwa zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike akizungumzia ushindi huo, amesema umetokana na
umahiri wa kuonesha shughuli mbalimbali zinazofanywa na vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Ufundi kwa kuoanisha taaluma na vitendo.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole Mbeya Sadick Rajab ubunifu na kujituma ndiyo nguzo muhimu ya Ushindi.
Maonesho hayo yaliyofanyika jijini Dodoma kwa wiki moja yalifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kufungwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako.
Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ufundi vilivyo chini ya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii vimeibuka kidedea
miongoni mwa vyuo 42 katika Kundi la Biashara, Utalii na Mipango.