Na Mwandishi wetu, Mirerani
WABUNGE wawili wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, Regina Ndege na Yustina Rahhi, wamekabidhi makabati 20 ya kuhifadhi dawa na vyakula vya wagonjwa na shilingi milioni 1 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya kituo cha afya Mirerani Wilayani Simanjiro.
Wabunge wao wametoa misaada hiyo mji mdogo wa Mirerani, kwenye ziara yao ya kutimiza ahadi yao baada ya kufika mwanzoni kwa mwaka huu na kukutana na changamoto hizo.
Ndege amesema wametekeleza ahadi yao baada ya kutembelea kituo cha afya kwenye maadhimisho ya kuzaliwa CCM na kubaini changamoto hizo.
“Mimi na mbunge mwenzangu Yustina Rahhi tumejitolea shilingi milioni 1 na vikabati hivyo 20 vya kuhifadhia vyakula, dawa na vitu vingine vya wagonjwa kwenye kituo cha afya Mirerani,” amesema Ndege.
Amewahakikishia viongozi wa eneo hilo kuendelea kushirikiana katika suala zima la kufanikisha maendeleo yanapatikana.
Kwa upande wake, Rahhi amesema wamefanikisha hilo na wanashukuru viongozi na wanawake wa eneo hilo walivyowapokea kwenye ujio wao.
“Tutaendelea kuwa pamoja katika kuhakikisha tunafanikisha maendeleo ya mkoa wetu wa Manyara ambao wananchi wake wengi ni wakulima na wafugaji,” amesema Rahhi.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amewashukuru wabunge hao kwa kutoa shilingi milioni 1 za ujenzi wa wodi na vikabati vya kuhifadhia vifaa tiba vya wagonjwa.
“Sisi kama wenyeviti wa mitaa ya mji mdogo wa Mirerani, tulianza kwa kuchanga shilingi milioni 5 za vyumba vitatu vya wodi hivyo tunawashukuru kwa kutuunga mkono,” amesema Kobelo.