Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi mwelekeo wa hali ya hewa kwa Tanzania kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Agosti 2021, taarifa hiyo imeelezea athari zinazoweza kujitokeza pamoja na ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Akizungumzia msimu huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi
kufuatilia utabiri huo wa msimu wa Juni-Agosti (JJA) 2021, hasa ikizingatiwa kuwa katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali wa Kusi vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.
“Kwa kawaida msimu wa kipupwe hutawaliwa na upepo wa Kusi, kutokana na matarajio ya uimarikaji wa wastani wa mgandamizo mkubwa wa hewa kusini mwa Afrika vipindi vichache vya upepo mkali vinatarajiwa kujitokeza. Hata hivyo, katika kipindi cha miezi ya Juni na Agosti, 2021 vipindi vya upepo mkali vinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi”. Alisema Dkt. Kijazi.
Akizungumzia hali ya baridi hususan maeneo yenye miinuko, Dkt. Kijazi alisema, Vipindi vya baridi kali vinatarajiwa hususan nyakati za usiku na asubuhi na vipindi vya baridi kali zaidi vinatarajiwa kujitokeza mwezi Julai 2021.
“Hali ya baridi inayotarajiwa kuwa chini ya nyuzi joto 6 hususan maeneo yenye miinuko katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe pamoja na maeneo ya kusini ya mkoa wa Morogoro, hivyo, inaweza kuleta athari kwa binadamu, wanyama, samaki pamoja na ustawi wa mazao mashambani hususani mazao ya muda mrefu kama migomba yanaweza kupata magonjwa ya fangasi na kudhoofisha ustawi wake.
Hali hii imesababishwa na hali ya joto katika bahari ya Hindi kuwa juu ya wastani, ongezeko la tija katika shughuli za uvuvi katika kipindi cha msimu huu linatarajiwa”. Alizungumza Dkt. Kijazi.
Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa, kwa ujumla hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya kawaida katika maeneo mengi ya nchi, hata hivyo, maeneo ya Ukanda wa Pwani
(Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), Nyanda za juu kaskazini mashariki (Kilimanjaro, Arusha na Manyara), ukanda wa Ziwa Victoria na magharibi mwa nchi (Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Rukwa, Katavi na Kigoma), hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa ya juu kidogo ya kiwango cha kawaida.
Kwa upande wa maeneo ya kanda ya kati (Singida na Dodoma), nyanda za juu kusini magharibi(Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe) na mkoa wa Ruvuma hali ya joto la chini inatarajiwa kuwa chini kidogo ya joto la kawaida kama
ilivyozoeleka.
Akizungumzia kuhusu mvua, Dkt. Kijazi alisema, vipindi vya Upepo wa Matlai vinatarajiwa kuleta unyevunyevu kutoka katika bahari ya Hindi na kusababisha kuwepo na matarajio ya vipindi vifupi vya mvua nyepesi katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, pamoja na ukanda wa Pwani (Mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara).
Aidha, katika ukanda wa Ziwa Victoria vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache.
Kwa upande wa athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema, Hali ya ukavu, upepo na ubaridi inaweza kusababisha athari kwa binadamu, wanyama na mazao
hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua za tahadhari ikiwa ni pamoja na kuzingatia matumizi mazuri ya maji na kujikinga ili kupunguza athari mbaya zinazoweza
kusababishwa na hali ya hewa inayotarajiwa.
Kwa taarifa zaidi tembelea; www.meteo.go.tz