********************************
Na Silvia Mchuruza
Biharamuro,Kagera.
Jeshi la polisi mkoani Kagera linaendelea kufanya uchunguzi wa vifo vya watoto wawili vilivyotokea wilayani Biharamulo Mkoa wa Kagera baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
Akizungumza na waandishi wa habari mei 28 mwaka huu Kamanda wa Polisi mkoani humo, Revocatus Malimi amewataja watoto hao kuwa ni Daniel Joseph (14) na Charles Njora (16) waliofariki Mei 27, 2021 wakati wakichunga ng’ombe.
Ameeleza kuwa waliokota chuma na kuanza kukichezea lakini kililipuka na kusababisha vifo vyao.
“Tunafanya uchunguzi ili kubaini kama chuma hicho kilikuwa ni bomu na kilifikaje katika maeneo hayo. Watoto hao walikuwa wakijiandaa kurejea nyumbani baada ya kumaliza kuchunga mifugo.”
“Hawakujua, walipokiona chuma hicho walianza kukichezea na kililipuka na kuwachana maeneo mbalimbali mwilini,” amesema.
Amewatahadharisha wazazi wanapobaini watoto wao wanachezea vyuma ambavyo hawavitambui watoe taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama.