…………………………………………………………………..
Na Richard Mwamakafu
Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) kimeiomba Serikali kuingilia kati usimamizi wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho unataofanyika Juni, 26, mwaka huu ili haki itendeke.
Mwenyekiti wa TWFA, Bi. Amina Karuma ametoa ombi hilo leo Mei, 26, 2021, Jijini Dodoma wakati alipokutana na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Gekul ofisini kwake.
Bi. Karuma amemwomba Mhe. Gekul kuuelekeza uongozi wa TFF na BMT kutoa ushirikiano kwa Chama hicho ili kufanya uchaguzi huru na haki kwa kuacha wanachama kumchagua Mwenyekiti wanayemtaka.
Aidha, Bi. Karuma amemwambia Mhe. Gekul kuwa TWFA kimepata mafanikio makubwa ambapo kiliweza kuanzisha Ligi Kuu ya Wanawake Nchini mwaka 2016 na pia kimewezesha kuandaa Timu ya Wanawake iliyoshinda mara mbili michuano ya kimataifa ikiwemo CECAFA na COSAFA.
Waziri Gekul amemuahidi kuwa, wizara yake itatoa ushirikiano wa kutosha ili kukuza mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake hapa nchini ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan la kuinua mchezo huo hapa nchini.