************************
NA MWANDISHI WETU, RUKWA.
KAMPUNI ya OCP Afrika iliyo kinara katika uzalishaji wa mbolea ulimwenguni, imezindua rasmi awamu ya pili ya mradi wa tathmini ya udongo ‘OCP SCHOOL LAB’ na kutoa elimu kwa wakulima juu ya afya ya udongo na mbinu sahihi kwa mazao husika hapa nchini.
Tukio hilo limefanyika mapema jana Mei 21, mjini Sumbawanga, wageni mbalimbali wakiwemo Wakulima, wasambazaji, wataalam wa Kilimo na viongozi wa Serikali walishiriki katika uzinduzi wa mradi huo uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Mhe. Kalolius Misungwi aliyewataka Watanzania kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Mhe.Misungwi ambaye alikuwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo wa Rukwa, Mhe. Joseph Mkirikiti, alisema kuwa, Sekta ya kilimo imeajiri asilimia 65 ya Watanzania wote na imelihakikishia taifa upatikanaji wa chakula kwa asilimia 100 pamoja na malighafi za viwandani, lakini bado idadi hiyo ya watanzania wanaojishughulisha kilimo haipo katika uwiano sawa na idadi ya watanzania wote hii ni kwa sababu ya tija ndogo inayotokana na uzalishaji mazao.
Ambapo pia alielezakuwa mpango wa upimaji wa udongo awamu ya pili utasaidia kuongeza na tija na bila shaka kuongeza uzaishaji wa mazao ya kilimo hasa katika Mkoa huo wa Rukwa.
“Niwapongeze sana kampuni ya OCP Afrika kwa kuandaa mradi huu ili kusaidia kutathimini rutuba ya udongo katika ngazi ya mkulima kwa vijiji 400 katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Iringa na Morogoro na kwamba kazi hiyo itafanyika bila malipo yoyote” Alisema, Mhe. Misungwi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya OCP Tanzania, Dkt. Mshindo Msolla alisema wanashirikiana na Serikali na kuandaa mchakato wa upimaji wa udongo kwa zaidi ya vijiji 100 ndani ya mkoa wa Rukwa lengo ni kupima udongo huo kwa wakulima bila gharama.
“OCP Tanzania kwa kushirikiana na Serikali tutaendesha zoezi la kuwaelimisha wakulima juu ya udongo wa eneo lao bila gharama zozote.
Majibu yatatolewa kwao pamoja na ushauri wa kitaalamu juu ya nini kifanyike ili kutunza ubora wa udongo wa kijiji husika kwa matokeo bora ya shughuli za kilimo” alisema Dkt. Msolla.
Ambapo aliongeza kuwa, Katika kila kijiji zaidi ya wakulima 100 watafikiwa na kuelimishwa namna bora za kufanya kilimo kiwe cha mahindi, mpunga au alizeti kulingana na maeneo waliopo huku mradi huo ukitazamia kufikia wakulima 10,000 kwa mkoa wa Rukwa pekee.
“Ni jambo lenye ulazima, kwamba wakulima wetu wawe rafiki wa teknolojia za kisasa zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji wao, na hivyo kuondokana na umasikini.
Mradi huu wa upimaji na tathmini ya udongo ni jambo la kipekee sana na hivyo tunahamamisha wakulima wote wawe sehemu ya mradi huu”. Aliongeza Dkt. Msolla.
Aidha, Dkt. Msolla alisema wanatarajiwa kutoa tathmini ya udongo na mapendekezo ya matumizi ya mbolea kwa wakulima wapatao 14,000 watakao wakilisha wakulima wenzao kutoka mashamba mbalimbali kwa kutumia technolojia ya kisasa.
Mradi huo wa upimaji na tathmini ya udongo kwa mwaka 2021, Unatarajiwa kuendeshwa katika vijiji 400 na kuwafikia wakulima wapatao 40,000 kufikia mwisho wa mwaka 2021.
OCP Afrika kupitia kampuni tanzu ya OCP Tanzania, ilizindua awamu ya kwanza mradi wa tathmini ya udogo mwaka 2019, na awamu hii ya pili ya mradi huo uliozinduliwa jana Mei 21, unatarajiwa kuhudumia wakulima na wadau wa kilimo wa mikoa ya Rukwa, Morogoro, Mbeya na Iringa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Idara za Kilimo (taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) kituo cha Uyole) na Wizara ya TAMISEMI.
Mradi huu ni mwendelezo wa awamu ya kwanza iliyozinduliwa mwaka 2019 na kufikia wakulima na wadau wa kilimo 20,000 katika mikoa za Njombe na Songwe ambapo majibu ya utafiti wa udongo kwenye mikoa hiyo yameweka bayana kwamba ukiachia mbali upungufu wa madini ya Fosforas na Naitrojeni uliopo kwa kipindi kirefu, kuna upungufu pia wa madini ya Zinki, Salfa pamoja na Potasiamu.
OCP Afrika ilianzishwa mwaka 2016, ambapo tangu 2017 zaidi ya wakulima 390,000 wamenufaika na miradi ya upimaji na tathmini wa udongo kutoka nchi nane (8) barani Afrika ikiwemo Naijeria, Togo, Ghana, Guinea, Kenya, Burkina Faso, Cote D’Ivoire na Senegal huku Tanzania ikiungana na nchi hizo kuwa moja wa nchi wanufaika wa mradi huo
kwa ushirikiano na Serikali kupitia Wizara ya kilimo, TAMISEMI pamoja na Taasisi ya utafiti wa Kilimo (TARI).
Kampuni hiyo yenye makao yake makuu nchini Morocco, kampuni ya OCP Afrika ni kampuni tanzu ya OCP Group vinara wa uzalishaji wa mbolea ulimwenguni yenye uzoefu wa miaka zaidi ya 100.