Home Michezo MOUNT HANANG’ QUEENS KUTINGA LIGI KUU

MOUNT HANANG’ QUEENS KUTINGA LIGI KUU

0

*******************************

Na Mwandishi wetu, Manyara

 

TIMU ya soka la wanawake ya Mount Hanang’ Queens Sports Club ya Mkoani Manyara, imejipanga kuhakikisha inapanda daraja na kufikia Ligi kuu ya soka nchini.

 

 

Mwenyekiti wa timu ya Mount Hanang’ Queens Sports Club, Gisela Msoffe akizungumza juzi alisema timu hiyo ambayo ipo ligi daraja la kwanza itafanya jitihada za dhati ili kupanda ligi kuu.

 

 

Amesema lengo lao ni kuendeleza vipaji vya watoto wa kike, kuhemasisha mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake na jamii na kuwaweka karibu.

 

“Timu hii ilianzishwa mwaka 2018 na ina wachezaji 21, viongozi tisa, tunaomba wadau watuunge mkono kwa kuwashika mikono wasichana wa timu yetu kwani tunapambana kuhakikisha tunapanda daraja na namba ya akaunti yetu ni A/C 41010017131 benki ya NMB,” amesema Msoffe.

 

Amesema walishiriki mashindano mbalimbali ya ndani ya wilaya hiyo tangu mwaka 2018, mwaka 2019 walishiriki mashindano ya mkoa , mwaka 2020 walishiriki mashindano ya ligi daraja la kwanza wanawake na na mwaka huu ukimalizika wanatarajia kupanda daraja na kufikia ligi kuu.

 

“Hatuna chanzo maalum cha fedha kulingana na uchanga wetu, ila tunategemea sisi viongozi wa timu, wapenzi na mashabiki wa mpira, wahisani na mfadhili mkuu wa timu kwa sasa ni mdau wa maendeleo Paul Phares Mnyandwa,” amesema Msoffe.

 

 

Amesema mdhamini wao Mnyandwa hadi hivi sasa ameshiriki kutoa ufadhili kwa kuwapa posho shilingi elfu 50 kila mwezi kila mchezaji, zawadi kwa kushinda mchezo na Fountain Academy ya Dodoma, huduma ya chakula na uendeshaji wa timu.

 

Mfadhili wa timu ya soka ya Mount Hanang’ Queens Sports Club, Paul Phares Mnyandwa amesema ameamua kudhamini timu hiyo kwani anaupenda mpira wa miguu na alikuwa mchezaji kwenye miaka iliyopita.

 

Mnyandwa amesema hadi hivi sasa ameshiriki kutoa ufadhili kwa timu hiyo kwa kujitolea fedha zake shilingi milioni 2 laki saba na elfu 20.

 

Amesema alianza kucheza mpira akiwa na umri wa miaka 17 hadi 25 katika nafasi ya mshambuliaji namba tisa, akiwa mshabiki wa timu ya Yanga na anaupenda aliamua awadhamini wachaezaji wa timu hiyo ya wanawake.

 

“Nimeona sina kingine cha kuwapa watoto hawa wajukuu zangu kwani wazazi wao wamenipokea vizuri nikapata mashamba japokuwa mimi mtu wa Morogoro hivyo nawaunga mkono kwa kuwapa ufadhili huu,” amesema Mnyandwa.

 

Amesema kutokana na juhudi kubwa waliyoonyesha wachezaji hao anaamini siku moja kabla ya miaka mitatu ijayo watakutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kuzungumza naye juu ya mafanikio yake kwani ni mwanamke pekee hapa nchini anayependwa na watanzania.

 

Mkuu wa upelelezi na makosa ya jinai wa polisi Wilaya ya Hanang’ Amilton Matagi amesema michezo huchangia kuepusha uhalifi ikiwemo mimba za watoto.

 

Matagi amesema wao kama polisi wanashirikiana na jamii kupitia polisi jamii ili kukomesha uhalifu kwenye maeneo tofauti hivyo wanaposhiriki kwenye michezo uhalifu hupungua.

 

Amesema wasichana hao wameshajitambua kuwa michezo ni sehemu ya maisha yao na mtoto wa kike siyo chombo cha starehe ila anaweza akafanya mambo makubwa wakiwa na mfano wa Rais Samia ambaye ni mwanamke ila ni Rais wa nchi.

 

“Ili kuwaunga mkono wasichana hawa ambao wanacheza soka ninatoa shilingi elfu 25 kwa ajili ya kununua soda kreti mbili na nusu kwa ajili ya ninyi kunywa soda baada ya mazoezi yao,” amesema Matagi.

 

Nahodha wa timu hiyo, Tatiana Kabuka alimuomba Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul, ambaye ametokea Mkoani Manyara, kuitupia jicho timu hiyo.

 

 Kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Agatha Theofil amewashukuru wadau wote wanaoiunga mkono timu hiyo na wanawaahidi kuwa watajitahidi kupiga hatua hadi kufikia ligi kuu ya soka la wanawake.