*********************
Na Mwandishi Wetu,Morogoro
Serikali imewashauri wananchi kupeleka ramani zao za ujenzi kwa wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili waweze kupata ushauri wa kitaalamu katika miradi yao ya ujenzi lengo ikiwa ni kuepusha madhara pindi yanapotokea majanga ya moto.
Ushauri huo umetolewa leo na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya zimamoto katika Viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro
“Askari wetu wa Zimamoto wamekua wakipata shida kuyafikia maeneo na majengo mbalimbali pindi yanapotokea majanga mbalimbali ikiwemo moto,hali inayopelekea kuteketea kwa mali nz thamani mbalimbali,sasa natoa rai kwa wananchi kuwasiliana na wataalamu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili waweze kupata ushauri wa kitaalamu kupitia ramani zao za ujenzi “ alisema Chilo
Sambamba na ushauri huo pia Naibu Waziri huyo amewaomba wananchi kuwaunga mkono Jeshi la Zimamoto kwani kazi wanazofanya zinahitaji ujasiri mkubwa nani kazi za hatari huku akiwaasa kuchukua tahadhari za usalama dhidi ya majanga ya moto na mengineyo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,John Masunga alielezea dhana ya maadhimisho hayo kuwa ni kuenzi wahanga wote waliopoteza Maisha katika ajali za moto na kuwaezi kwa namna walivyojitoa katika kuokoa Maisha na mali za watu wengine huku wakihatarisha Maisha yao.
“Ni siku muhimu ikiwa tunawakumbuka wapendwa wetu basi tuchukue tahadhari kwa vyanzo mbalimbali vinavyosababisha majanga ya moto na yanayofanana na hayo na sisi jeshi la zimamoto tunajitahidi kutoa elimu mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wetu waelevu katika kuhakikisha maisha ya wananchi na mali zao zinakua salama” alisema Kamishna Jenerali John Masunga
Katika maadhimisho hayo maonesho mbalimbali yalionyeshwa yakihusiana na kinga na tahadhari sambamba na elimu ya maokozi ambapo wanafunzi kutoka shule za mkoani Morogoro kupitia Chama cha Skauti Tanzania walipata mafunzo hayo pia.