Home Michezo SIMBA JAMII YASAIDIA WATOTO YATIMA KITUO CHA UMRA,WAIOMBEA USHINDI KESHO

SIMBA JAMII YASAIDIA WATOTO YATIMA KITUO CHA UMRA,WAIOMBEA USHINDI KESHO

0
Watoto Yatima wa Kituo cha Umra kilichopo Magomeni wilayani Kinondoni wakiomba dua pamoja na baadhi ya wawakilishi wa Taasisi ya Simba Jamii Tanzania Enterprise (SJTE), ili kusaidia Klabu ya Simba kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa marudiano na timu ya Kaizer Chiefs.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Simba Jamii Tanzania Enterprise (SJTE), Patrick Mwanakatwe akikabidhi mashuka 30 kwa Muasisi wa Kituo cha Umra  Rahma Kishumba (katikati) na Mlezi wa Kituo hicho Thuwaybaty Ahmada Nassoro (kushoto) wengine ni watoto.
Muasisi wa Kituo cha Umra kilichopo Magomeni wilayani Kinondoni jijini Dar, Ramha Kishumba alielezea furaha waliopata kupatiwa msaada waashuka 30 kutoka Simba Jamii Tanzania Enterprise (SJTE), kutosho ni Mwenyekiti wa SJTE, Patrick Mwanakatwe.
……………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
TAASISI ya Simba Jamii Tanzania Enterprise (SJTE), imetoa msaada wa mashuka 30 kwa Kituo cha Kulea Watoto Yatima cha Umra kilichopo Magomeni Wilayani Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umekabidhiwa na Mwenyekiti wa SJTE, Patrick Mwanakatwe ambaye aliambata na Mjumbe wa Utendaji Mussa Mongi, Mlezi wa Hassan Mbilili na Mjumbe wa Kamati ya Habari na Matangazo Suleiman Msuya.
Akizungumza baada ya kutoa msaada huo Mwenyekiti wa SJTE, Mwanakatwe amesema dhamira ya taasisi hiyo pamoja na kuishabikia Klabu ya Simba ila wanahakikisha wanatatua changamoto za jamii kwa kujichangisha kidogo walichonacho.
Amesema kwa leo wametoa mashuka 30 kwenye kituo cha Umra ambacho kilikuwa kinahitaji hilo.
Mwanakatwe amesema wamekuwa wakitoa misaada kwa watoto yatima, watu wenye ulemavu kwa kuwapatia viti lengo likiwa ni kuwapunguzia adha mbalimbali.
“Simba Jamii Tanzania Enterprise ni taasisi ambayo inahusika na kuishabikia Klabu ya Simba na huduma za jamii kama kusaidia watoto yatima na wenye ulemavu wa viungo hivyo leo ni zamu ya Umra tunaendelea kujipanga kuendelea kusaidia makundi hayo kila kona ya nchi.
Mashuka 30 tuliyotoa hapa ni sehemu ya msaada wetu na tunaendelea kuchangishana tuweze kuwapatia mahitaji mengine kama magodoro ambayo bado wanahitaji,” amesema.
Mwenyekiti amesema SJTE ina wanachama kutoka pande zote dunia ikiwemo Japani, Afrika Kusini, Marekani, Uingereza, Tanzania na kwingineko.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati ya Utendaji SJTE, Mongi amewaomba wana Simba popote walipo duniani kujiunga na taasisi hiyo ili kuweza kusaidia jamii.
Mongi alisema kwa sasa wapo kwenye mikakati mbalimbali ya kuhakisha SJTE inatangazwa zaidi ili kufikia wana Simba wengi.
Mlezi wa Simba Jamii, Mbilili alisisitiza kuwa kupitia taasisi hiyo wameweza kusaidia watu wengi hivyo ni imani yao wataweza kufikia kundi kubwa.
Muasisi wa Kituo cha Umra, Rahma Kishumba amesema wanashukuru kupata msaada wa mashuka 30 kutoka Simba Jamii na kuwataka waendelee kusaidia makundi maalum.
Amesema Kituo cha Umra kina watoto yatima 117 ambao wamewapata katika maeneo mbalimbali hivyo kuwataka wadau wengine kuunga mkono juhudi zao za kulea watoto hao.
“Tunawapongeza SJTE kwa kuweza kutatua changamoto hii ya mashuka kwani ilikuwa inatuumiza vichwa ni imani yetu wengine watakuja kutupatia magodoro,” amesema.
Aidha, amesema watoto hao yatima waliopo kwenye vituo vyao vinne ambavyo ni Magomeni, Buza, Mbezi na Vikawe wanahitaji bima ya afya hivyo kuomba wadau kuwasaidia kwenye eneo hilo.
Kishumba amesema watoto hao yatima wanasoka katika shule mbalimbali jambo ambalo linasaidia kutimiza ndoto zao.
Muasisi huyo alitumia nafasi hiyo kuiombea ushindi timu ya Simba dhidi ya Kaizer Chief wanaotarajiwa kuchezwa kesho katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini hapa.
Kwa upande wao watoto Yasira Dauda na Abdul Hakimu Nassor wameishukuru SJTE kuwapatia zawadi hizo na kuahidi kuzitunza.
Aidha, watoto hao wameombea dua timu ya Simba iweze kuibuka na ushindi katika mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Timu ya Kaizer Chief.