Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni (Mb), akijibu swali bungeni kuhusu msamaha kwa wadaiwa wa kodi jijini Dodoma.
*********************************
Na, Saidina Msangi na Josephine Majura, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa katika Mwaka wa Fedha 2018/19 ilitoa msamaha kwa wadaiwa wa Kodi (Tax Amnesty) uliohusisha riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote yaliyolimbikizwa kwa miaka ya nyuma ili kuongeza makusanyo.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Yussuf Masauni (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mheshimiwa Henry Maganga Nicodemus, Mbunge wa Mbogwe aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kufuta madeni ya muda mrefu kwa wafanyabiashara wa ndani yatokanayo na ukosefu wa elimu juu ya matumizi sahihi ya mashine za EFD wanayodaiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania.
Mhe. Masauni alisema kuwa msamaha huo ulilenga kusamehe malimbikizo ya nyuma ya riba na adhabu (Interest and Penalties) kwa kiwango cha asilimia 100 kwa wafanyabiashara wote hapa nchini ambao walikuwa na malimbikizo ya madeni hayo ya kodi.
“Msamaha huo ulitolewa kwa kipindi cha miezi sita (6) kilichoanzia tarehe 1 Julai 2018 mpaka tarehe 31 Desemba 2018, kutokana na kusuasua kwa utekelezaji wake, Serikali iliongeza muda wa msamaha huo kwa miezi sita ili wafanyabiashara waliokuwa na madeni hayo wakamilishe malipo husika”alieleza Mhe. Masauni.
Aidha Mhe. Masauni alisema kuwa hatua hiyo ya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi SURA 438 ilitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali na kukusanya malimbikizo ya madeni ya nyuma ya kodi (Principal Tax) pamoja na kuinua kiwango cha ulipaji kodi kwa hiyari kwa zaidi ya asilimia 10.
Mhe. Masauni aliongeza kuwa licha ya nia nzuri ya Serikali ya kufuta riba na adhabu ili kuwawezesha walipakodi wenye madeni sugu ya kodi kuyalipa kwa awamu ili kurahisisha mwendelezo wa biashara zao wengi wao hawakulipa kodi hizo hata baada ya kuingia mikataba na TRA na hata baada ya Serikali kuongeza muda wa ziada wa kufanya malipo ya kodi husika yaliyotokana na msamaha huo.