Home Mchanganyiko RAIS MSTAAFU MHE. KIKWETE AONGOZA KONGAMANO LA MIAKA 40 YA JUMUIYA YA...

RAIS MSTAAFU MHE. KIKWETE AONGOZA KONGAMANO LA MIAKA 40 YA JUMUIYA YA SADC

0

Rais Mstaafu wa awamu ya nne Mhe.Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Maendeleo ya Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC lililofanyika katika leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine akiwasilisha salamu za Wizara kwa washiriki (hawapo pichani) katika kongamano la maadhimisho ya miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula. Kongamano hilo limefanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Prof. william Anangisye akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Maendeleo ya Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC lililofanyika katika leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Spika wa Bunge Mstaafu Mhe.Anna Makinda akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Maendeleo ya Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC lililofanyika katika leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Wadau mbalimbali wakiwa katika Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya Maendeleo ya Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC lililofanyika katika leo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

************************************

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ameongoza Kongamano la Maadhimisho ya miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na kutoa uzoefu na mchango wa Tanzania katika jumuiya hiyo.

Raisi Kikwete amesema kuwa lengo la kuanzishwa kwa SADC ni kupunguza utegemezi, kukuza ushirikiano utakaojenga utengamano wa kikanda, kuhamasisha utekelezaji wa sera za mipangi ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za pamoja katika mpango wa maendeleo na mpango wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama.

“Maadhimisho haya yanaadhimishwa na nchi zote wanachama wa SADC kwa lengo la kutoa fursa ya kuangalia na kutambua malengo, mchango na fursa zilizopo katika nchi wananchama wa SADC,“ amesema Dkt. Kikwete.

Dkt. Kikwete ameongeza kuwa wapigania uhuru kutoka nchi nyingi za Afrika wanaendelea kuikumbuka Tanzania kutokana na mchango mkubwa wa kuanzisha harakati za kuzikomboa nchi nyingine kutoka katika utawala wa kikoloni ikiwa ni pamoja na Tanzania kuwapatia mbinu za kupambana na Wakoloni.

Awali akiwasilisha salamu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa niaba ya Mhe. Waziri, Balozi Liberata Mulamula (Mb), Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine amesema kuwa maadhimisho ya miaka 40 ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) amesema pamoja na masuala mengine, yanalenga kuenzi mchango mkubwa wa Viongozi Wakuu waanzilishi wa SADC ambao maono yao yaliweka msingi wa ukombozi wa kisiasa na kiuchumi kwa Kanda ya Kusini mwa Afrika; na Kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu mtangamano wa SADC na faida za uanachama wetu kwenye Jumuiya hii ikiwa ni pamoja fursa zilizopo katika Nyanja mbalimbali ili waweze kuzichangamkia.

“Tunapoadhimisha miaka 40 ya SADC hatuwezi kamwe kuepuka kuzungumzia mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania kwenye Jumuiya hii.  Itakumbukukwa kuwa, Tanzania wakati wa uongozi wa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ilifanya kazi kubwa ya kusaidia harakati za ukombozi hususan kwa nchi za Kusini mwa Afrika. Kadhalika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa Mwenyekiti wa Kwanza wakati wa SADCC kabla ya kubadilishwa kuwa SADC mwaka 1992,” amesema Balozi Sokoine

Ameongeza kuwa Uenyekiti wa Tanzania katika SADC kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma, ulikuwa wa mafanikio kwa nchi na kwa Kanda kwa ujumla. Miongoni mwa mafanikio makubwa tunayojivunia ni kuridhiwa kwa Lugha yetu ya Taifa, Kiswahili kuwa miongoni mwa Lugha nne za SADC.

“Ili SADC itimize malengo iliyojiwekea ya kuwa Jumuiya yenye amani, usalama, ustawi na maendeleo kama ilivyoelezwa kwenye Dira ya SADC ya mwaka 2050 (SADC Vision 2050) na Mpango Mkakati wa Maendeleo wa Kanda 2020 – 2030 (Regional Indicative Strategic Development Plan – RISDP), kila mdau lazima atimize wajibu wake umpasao,” amesema Balozi Sokoine.

Nae Spika wa Bunge Mstaafu Mhe. Anna Makinda amesema kuwa nchi wanachama nyingine zinakiri na kutambua mchango wa Tanzania katika harakati za kuzikomboa kutoka kwenye utawala wa kikoloni. “Nchi hizo zimekuwa zinakiri kuwa bila Tanzania kuzisaidia zingechelewa kupata uhuru ikiwemo Afrika Kusini ambayo katika jitihada za kutafuta Uhuru wake ilimwaga damu,” amesema Mhe. Makinda.

Pamoja na hayo Mhe. Makinda amesema kuwa mchango wa Hayati Mwalimu Julius Nyeyere utaendelea kukumbukwa daima na nchi wananchama wa SADC.