***********************************
Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo inatarajia kuadhimisha Siku ya Uanuai wa Utamaduni Duniani kesho tarehe, 21 Mei, 2021, kwa kufanya Kongamano la kihistoria kwenye nchi yetu la kuenzi mchango wa Tanzania katika harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika katika Ukumbi wa JNICC Jijini Dar es Salam.
Kongamano hilo litafunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) na linatarajiwa kuhudhuriwa na wadau mbalimbali watakao jadili mada za kutambua, kuenzi na kutangaza urithi wa ukombozi wa Afrika ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa Tanzania katika Ukombozi wa Bara la Afrika.
Mwaka 2011, Tanzania ilikasimiwa uratibu wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Afrika ili kuhifadhi, kulinda na kutafiti masuala ya ukombozi wa Bara la Afrika.
Hivyo, Kongamano hili ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Afrika. Ambapo matokeo yake yanatarajiwa kuamsha ari ya ujifunzaji wa somo la historia ya ukombozi wa Afrika kwa Vijana na kuenzi mchango wa waasisi wa harakati za ukombozi wa Afrika waliopo hai na waliotangulia mbele za haki.
Kongamano hili litakuwa sehemu ya kutambulisha zao jipya la utalii wa kiukombozi kwa kuyanadi maeneo zaidi ya 250 ya urithi wa ukombozi yaliyopo nchini. Utalii huu utakuwa sehemu ya ukombozi wa kiuchumi na kifikra kwa watanzania wote.
Kongamano hili litahamasisha watanzania kutembelea Makumbusho ya Urithi wa ukombozi iliyopo mtaa wa Garden Avenue, Mkabala na Ubalozi wa Kanada ambapo zipo Ofisi ya Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Afrika.
Baada ya maadhimisho ya Kongamano, tarehe 22- 23 Mei 2021, kutakuwa na kikao kazi cha maafisa Utamaduni na Michezo toka katika Mikoa na Halmashauri zote nchi nzima. Lengo la kikao kazi hicho ni kujadili maendeleo, fursa na changamoto zinazoikabili sekta hizi na kupendekeza njia ya utatuzi wake.