Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akitoa Zawadi ya Eid El Fitri kwa watoto wa Makao ya Kisedet Jijini Dodoma alipomwakilisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, Wazee na watoto, Dkt. Dorothy Gwajima.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akiwa na wototo wa Makao ya Kisedeti jijini Dodoma alikokwenda kutoa zawadi ya Eid El Fitri kwa kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, Wazee na watoto, Dkt. Dorothy Gwajima.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi akiangalia mradi wa bwawa la samaki wa Makao yawatoto Kisedeti unaowasaidia kuongeza kipato cha kuendesha kituo hicho kilichopo eneo la Chigongwe jijini Dodoma.
………………………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Dodoma
Wamiliki wa Makao ya watoto wametakiwa kuhakikisha watoto wanaohudumiwa katika Makao hayo wanatengamanishwa na familia zao badala ya kubaki katika makazi hayo kwa muda mrefu.
Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’ondi ametoa agizo hilo wakati akitoa zawadi ya Siku kuu ya Eid el Fitr kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima kwa watoto wa Makao ya Kisedet Jijini Dodoma.
Amesema wajibu mkubwa wa makao hayo ni kuwasaidia watoto kutatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja ja na kuwatangamanisha (kuwarejesha) kwenye familia ili waendelee kulelewa kwa utaratibu wa kawaida.
“Tunapowachukua watoto hawa na kuwaleta kwenye huduma hizi ni lazima kila mtoto awe na mpango wake wa kumtengamanisha kikamilifu, watoto wasikae kwenye makao muda wote, kila mtoto afanyiwe tathmini binafsi ya mahitaji yake anapoingia tu” alisisitiza Dkt. Ng’ondi
Aliongeza kuwa lengo ni kupunguza idadi ya watoto wanaoishi kwenye makao nchini na kuwawezesha kupata haki ya kuishi na familia zao ambazo ndiyo sehemu bora kwao kwa malezi na makuzi.
Aidha, Dkt. Ng’ondi amesema Serikali itasaidiana na makao yote ya watoto nchini kuhakikisha familia zinaelimishwa kuhusu njia bora za malezi ambazo hazihitaji ukatili ili watoto wasione sababu ya kukimbilia mitaani.
“Kuishi mitaani tunaweza kudhani ni kitu cha kawaida lakini ukiongea na watoto wenyewe kuishi mitaani hawakupenda” aliongeza Ng’ondi.
Kwa upande wa watoto wa makao hayo wamemshukuru Waziri Gwajima kwa zawadi, pia wamewashauri watoto wenzao wanaolelewa kwenye makao kupenda kurudi nyumbani kwao ili wapate malezi ya familia.
Siku Kuu ya Idd El Fitr huadhimishwa kimataifa ikiwa baada ya kuhitimisha nguzo muhimu ya Kiislam ya kufunga katika mwezi wa Ramadhani.