Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dkt. Simon Chacha akiongea wakati wa kikao kazi hicho ambacho kilifanyika Kwenye ukumbi wa RAS Kigoma.
Na. Catherine Sungura, Kigoma
Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) una lengo la kuhakikisha jamii yote ya watanzania wameondokana na athari za magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030 ambapo Tanzania kampeni ya kudhibiti magonjwa hayo yalianza mwaka 2009.
Hayo yamebainishwa leo na Mratibu wa taifa wa Mpango huo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. George Kabona wakati wa kikao kazi cha uraghibishaji na uhamasishaji kwa viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri za mkoa wa kigoma.
Dkt. Kabona amesema kuwa kati ya magonjwa 13 ambayo Mpango huo wanapambana nayo,magonjwa matano ya Usubi, Takoma, Matende na Mabusha, Kichocho na Minyoo ya Tumbo yamepewa kipaumbele katika utekelezaji wa shughuli za kuyadhibiti na kwa maana hiyo yanatakiwa kudhibitiwa mapema kwa njia ya kugawa kingatiba ngazi ya jamii pamoja na watoto mashuleni.
“Kwa kupitia takwimu zilizopom Shirika la Afya duniani(WHO) liligundua kwamba magonjwa Yaliyokuwa hayapewi kipaumbele yameathiri sana jamii kwa kiasi kikubwa na takribani watu wapatao bilioni 2 walikuwa kwenye hatari ya kupata madhara ya magonjwa haya na hatimaye kuishi maisha ambayo watashindwa kuzalisha mali na kuwa mzigo kwa jamii hivyo ikaja na mpango mkakati wa kupambana na kudhibiti magonjwa hayo”.
Dkt. Kabona alitaja mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti magonjwa hayo kuwa ni pamoja na ugawaji wa kingatiba kwa magonjwa yote matano kufanyika katika maeneo yote nchini kwa asilimia 100. “Kwa upande wa Matende naMabusha kati ya halmashauri 119 zilizokuwa zimeathirika hadi kufikia mwaka huu ni halmshauri 7 tu ndio bado zimebaki na tatizo hilo na kama Wizara wanaimarisha mkakati wa kumaliza kabisa tatizo hilo”.
Kwa upande wa ugonjwa wa Trakoma (Vikope) amesema kulikuwa na halmashauri 71 zilizoathirika na kwa sasa zimebaki halmshauri sita tu ambazo kati ya hizo halmashauri mbili za Kongwa na Chamwino ugonjwa umerudi baada ya kufaulu kupunguza maambukizi miaka miwili iliyopita na kufuatia kurudi huko kwa ugonjwa hivyo wanaendelea kufuatilia sababu zake kwa kufanya tafiti za kiutendaji na taarifa itatolewa hivi karibuni.
Hata hivyo Dkt. kabona aliwataka wananchi kujenga tabia ya kufanya usafi wa uso ,matumizi wa vyoo pamoja na usafi wa mazingira kwa dhumuni la kuzuia mazalia ya inzi ili kuweza kujikinga na ugonjwa wa trakoma
Amesema pia Ugonjwa wa Kichocho na minyoo ya tumbo umeathiri halmashauri zote 184 kwa kiwango tofauti tofauti. Dr Kabona ameongeza kwa kusema kuwa zipo athari za magonjwa hayo ambazo husababisha utegemezi kwa jamii na kusababisha ndugu wa karibu kushindwa kuzalisha mali kwa sababu ya kutumia muda mwingi na rasilimali kuwahudumia wagonjwa wao.
Amesema pia kuwa toka mwaka 2008 Mpango umeweza kutoa huduma ya upasuaji wa Mabusha kwa wagonjwa zaidi ya 6000 na huduma hiyo bado inahitajika kwa kiwango kikubwa hasa mikoa na halmashauri za ukanda wa Pwani
kwa ajili ya kuzuia mazalia ya Inzi na hatimaye kutokomeza kabisa magonjwa hayo . Awali akifungua kikao kazi hicho Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ambaye ni Katibu Tawala wa mkoa huo Bw. Rashid Mchatta amesema kila halmashauri zinatakiwa kufikia malengo ya asilimia 80 ya umezeshaji kingatiba hizo na kuwataka viongozi wa mkoa, wilaya na halmashauri kushirikiana kwa kubadilishana mawazo jinsi ya kutatua changamoto ili kila mmoja aweze kuwafikia watoto wote waliolengwa kwa kutoa elimu kwa jamii na kuhamasisha wazazi na walezi.