Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda akizungumza na Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo (ASA) mkutano uliofanyika leo Mei 11, 2021 Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda akizungumza na Menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo (ASA) mkutano uliofanyika leo Mei 11, 2021 Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda akimkabidhi cheti cha shukrani Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya ASA aliyemaliza muda wake Dkt. Ashura Kihupi leo Mei 11, 2021 Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda akimkabidhi cheti cha shukrani Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge, leo Mei 11, 2021 Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.
Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo (ASA) leo Mei 11, 2021 jijini Dodoma.
*************************
Waziri wa Kilimo Prof. Aldof Mkenda ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Mbegu (ASA ) pamoja na Bodi mpya inayotarajiwa kupatikana hivi karibuni kufufua mashamba 13 ya kuzalisha mbegu bora na kuweka miundombinu ya umwagiliaji ili kuahakikisha yanazalisha kwa tija ili kuwasaidia Wakulima kupata mbegu bora; Kwa wakati na kwa bei nafuu.
Waziri Mkenda amesema leo Mei 11, 2021 Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma wakati akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi ya (ASA) iliyomaliza muda wake pamoja na Menejimenti ya kuwa uzalishaji wa mbegu bora ni lazima uende sambamba na matumizi ya maji ili kuhakikisha mbegu zinazalishwa kwa bei nafuu.
Prof. Mkenda amesema uzalishaji wa mbegu bora kwa mwaka ujao wa fedha ni kipaumbele cha Wizara hiyo ni katika uzalishaji wa mbegu bora kupitia mashamba hayo ndio maana Wizara imeamua kuanzisha Mfuko Maalum wa Kilimo ambao unataraji kugharamia shughuli mbalimbali za maendeleo ya Sekta ya Kilimo, mbegu ni eneo moja wapo.
Waziri Mkenda amesema ili kuongeza tija Wakala wa Mbegu Bora za Kilimo (ASA) inatakiwa kufunga miundombinu hiyo ya umwagiliaji ili kuongeza tija kwenye upatikanaji wa mbegu bora.
“Tuyafufue mashamba yote 13 ya ASA na yafungiwe miundombinu ya umwagiliaji na kwa sababu Tume ya Maendeleo ya Umwagiliaji ipo chini ya Wizara ya Kilimo; Na tumeelekeza hakuna kuanzisha Mradi mpya wa umwagiliaji mpaka tuwe tumemaliza kujenga miundombinu ya umwagiliaji kwenya mashamba yote ya ASA.” Amesisitiza Waziri Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa njia pekee ya kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa bora ni kuongeza tija kwenye kilimo kwa kuhakikisha mbegu bora zinapatikana kwa bei nafuu ili Wakulima wazitumie kuzalisha kwa tija na kwa kufanya hivyo mazao ya chakula yatapatikana kwa wingi na kwa bei nafuu. Jambo hilo litachangia kupunguza gharama za maisha na kwa ajili hiyo. Wananchi wengi watanunua chakula kwa bei nafuu.
Waziri Mkenda amesema uzalishaji wa tija kwenye mbegu za mafuta utasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kutokana na kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi ambapo Serikali imekuwa ikitumia zaidi ya nusu tilioni kuagiza mafuta kutoka nje.
Pia Prof.Mkenda amesema kuwa ipo haja kwa Serikali kuwa msimamo unaoakisi kauli mbiu ya kilimo ni uti wa mgongo ili Wakulima walime kwa tija na kuondokana na umaskini miongoni mwao.
“Tunaweza kuwa kwenye uchumi wa kati na hata kufikia uchumi wa juu lakini wimbi la umaskini likaendelea kwa Wananchi na tukawa tegemezi wa chakula; Lakini pia hatuwezi kuwa na mageuzi ya viwanda bila kufanya mageuzi ya kilimo hususani katika suala la uzalishaji wa mbegu.” Amesisitiza Waziri Mkenda.
Hata hivyo amesema kuwa ni lazima mashamba yote ya ASA yafufuliwe kwa kuwa utegemezi wa mbegu kutoka nje ya nchi wakati mwingine hausaidii kilimo cha hapa nchini.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya ASA, Dkt. Ashura Kihupi amesema kuwa zipo kero kubwa kwenye Sekta ndogo ya Mbegu ni uwekezaji mdogo uliofanywa pamoja na mtaji mdogo kwa ajili ya kuzalisha mbegu.
Dkt. Kihupi ametoa mfano wa shamba la mbegu la Msimba lililopo Kilosa mkoani Morogoro; Kuwa uzalishaji umekuwa mdogo kwa sababu hakuna miundombinu ya umwagiliaji maji.