Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),akizungumza na waandishi wa habari Leo Mei 8,2021 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Mwenendo wa Mamlaka za Maji Katika Utoaji wa Bili za Maji.
……………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji hapa nchini EWURA imesema imebaini baadhi ya mamlaka za maji kukiuka sheria zinazosimamia mamlaka hizo katika kutoa huduma kwa wananchi ikiwamo kutoza bei ambazo hazijapitishwa na EWURA na ubambikiziwaji wa bili za maji.
Hayo yamebainishwa Leo Mei 8,2021 jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Mhandisi Godfrey Chibulunje wakati akizungumza na wanahabari amesema baada ya kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wateja waliamua kufanya ukaguzi katika mamlaka 24 kati ya 94 zilizopo.
Amesema katika ukaguzi huo wamebaini mamlaka zote 24 zinamapungufu makubwa katika utoaji huduma kwa wananchi ikiwamo ubora wa mita za maji, taratibu za usomaji wa mita, ukokotoaji wa bili za wateja na utaratibu wa kutatua kero za wateja.
“mnamo January 7, 2021 EWURA ilisimamisha matumizi ya bei zote mpya zilizokuwa zianze kutumika mwaka 2021 kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa watumiaji wa maji ikiwamo ubambikiziaji wa bili na usomaji wa mita usiokuwa shirikishi tukaamua kufanya uchunguzi,
“katika uchunguzi huo tumebaini udhaifu katika usomaji wa mita, baadhi ya wasomaji wanakosa umakini na tatizo hili limeonekana kwa mamlaka zote 24 zilizochunguzwa, pia baadhi ya mamlaka kutoza bili za maji kwa kukadiria kutokana na kuharibika kwa mita” amesema Mhandisi Chibulunje.
Amezitaja Mamlaka za maji 24 ambazo wamezifanyia ukaguzi wa kina kuwa ni Kigoma, Bukoba, Babati, Moshi, Arusha, Tanga, Geita, Shinyanga, Kahama, Dodoma, Iringa, Musoma, Mbeya, Njombe, Songea, Vwawa-Mlowo, Mugango-Kiabakari, Bunda, Makambako, Sengerema, Muleba, Mwanhunzi, Gairo na Ngara.
Amesema baadhi ya Mamlaka za maji zimekuwa na uzembe katika usimamizi wa bei za maji zinazotozwa kwa wateja kwenye magati ambapo mamlaka hizo zilibainika bei za juu ya zile zilizoidhinishwa na EWURA mamlaka hizo zikiwa ni Mbeya, Makambako, Songea Tanga, Iringa, Shinyanga, Kahama, Geita Arusha, Moshi, Babati, Ngara na Kigoma.
Pia amesema wamebaini kuwa baadhi ya mamlaka hazitoi taarifa kwa wateja inapotokea kuwepo kwa mgao wa maji na hivyo kuleta usumbufu kwa wateja wao, mamlaka nyingi zimeacha jukumu la kutoa elimu kwa wateja juu ya huduma za maji ikiwamo haki ya mteja.
Ametaja baadhi ya hatua ambazo zimechukuliwa na EWURA katika mamlaka zenye mapungufu kuwa imezipiga faini mamlaka za maji Tanga na Babati kwa kuwauzia wananchi maji kwa bei ambayo haijaidhinishwa na EWURA na kuagiza mamlaka hizo kurudisha fedha za ziada zilizotozwa kwa wateja.
EWURA imezipelekea maagizo mamlaka za maji Mbeya, Songea, Makambako, Mwanhunzi na Gairo na kutaka zijieleze kwanini zisichukuliwe hatua kwa kukiuka maagizo ya EWURA, pia katika mwezi May imeziandikia baadhi ya mamlaka kwa kutoza bei kubwa katika magati.
EWURA imezitaka mamlaka zote kuhakikisha wanafanyia marekebisho katika dosari zote huku akibainisha kuwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Babati, Kigoma na Tanga taarifa zao zitawasilishwa katika mamlaka zao za uteuzi kutokana na kujirudia kwa makosa mara kwa mara.