********************
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ameyakumbuka makundi maalum ya watu wasiojiweza ya wazee, yatima na wajane katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kugawa futari ili kuunga mkono juhudi za waumini hao wa dini ya kiislam katika kukamilisha nguzo muhimu ya dini hiyo ya Swaum kati ya zile tano zilizoamrishwa na mwenyezi Mungu mtukufu
Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi futari hiyo Katibu wa ofisi ya Mbunge Ndugu Kazungu Safari Idebe amesema kuwa Mbunge Dkt Angeline Mabula anaamini kuwa jamii yenye hofu ya Mungu ni jamii iliyostaarabika, ni jamii yenye amani na upendo na inakuwa rahisi kwa jamii hiyo kuweza kujiletea maendeleo sanjari na kusisitiza juu ya kuiombea nchi na viongozi wake wote chini ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan
“Tunapokuwa katika mfungo tunakuwa karibu sana na Mungu, Tutumie mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kuiombea nchi yetu na viongozi wake, Tukifanya hivyo tutasonga mbele”. Alisema
Hajjat Fatma Lusendela ni mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake wa kiislam (JUWAKITA) chini ya baraza kuu la waislam Tanzania (BAKWATA) kwa wilaya ya Ilemela ambapo amempongeza na kumsifu kiongozi huyo kwa namna anavyoshirikiana nao, anavyojali na kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo hasa wajane, yatima na wazee kwani kila mwaka amekuwa akitoa sadaka hiyo ya futari kwa waumini wa dini ya Kiislam na hivi karibuni aligawa vitabu vya Qur an tukufu (Masaafu) kwa madrasa za jimbo hilo na misikiti
Nae Bi Aisha Hussein mkazi wa Kirumba kati akawataka viongozi wa ngazi mbalimbali na maeneo tofauti nchini kuiga mfano wa kiongozi huyo katika kuunganisha wananchi bila kujali tofauti zao na kushirikiana nao katika kutatua changamoto zinazowakabili.