Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya ndege Tanzania katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ACP Jeremia N. Shila (wa kwanza kutoka kulia) akionyesha jino la tembo lenye uzito wa kilo gramu 1.458 wakati akizungumza na waandishi wa Habari Leo jijini Dar es Salaam.
…………………………………………………………………………………
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi kikosi cha Viwanja vya ndege Tanzania katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wamefanikiwa kuwakamata watu nne katika matukio mawili tofauti likiwemo mtanzania mwenye uraia wa Marekani kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Kamanda wa Polisi Viwanja vya ndege Tanzania, ACP Jeremia N. Shila, amesema kuwa katika tukio kwanza Mei 3 mwaka huu majira ya saa 2:55 usiku katika Uwanja wa ndege wa JNIA, Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamefanikiwa kumkamata Bi. Marry Mzumbi Daniel (54) raia wa Marekania.
Mtuhumiwa Bi. Daniel alikamatwa katika eneo la ukaguzi wa mizigo ya abiria katika jengo la tatu wanaosafiri kwenda nje ya Nchi katika uwanja wa ndege wa JNIA ambapo alikamatwa akiwa na kipande kimoja cha jino la tembo kilichochongwa kama kinyago na kupigwa msasa na chenye uzito wa kilo gramu 1.458.
“Kipande hicho cha jino la Tembo kilikuwa kimefichwa kwenye begi lake la nguo na baada ya ukaguzi na upekuzi ndipo kilikutwa kipande hicho cha kinyago” amesema ACP Shila.
Amefafanua kuwa baada ya mahojiano mtuhumiwa alikiri kuwa ni kipande cha pembe ya ndovu ni mali yake ambayo alipewa na mama yake mzazi kabla hajafariki kama urithi wake, uku akibainisha kuwa mtuhumiwa anashikiliwa na uchuguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.
Katika tukio la pili Kamanda ACP Shila amesema kuwa Mei 6 mwaka huu majira ya saa 10:00 jioni katika kiwanja cha ndege cha JNIA wamewakamata abiria watatu wa Tanzania ambao ni Abdulaziz Abubakar Chende (26), Shaeeb Rashid Hamad (43), pamoja Sylivia Erick Kisamo (30) kwa tuhuma za kuwashawishi abiria wengine kukataa kufanyiwa kipimo cha COVID 19 na kulipa USD 25 kama ilivyoagizwa na Serikali.
Uchuguzi wa shauri unaendelea ili kubaini kama kuna jinai imetendeka na pindi itakapothibitika watuhumiwa hao watafikishwa Mahakamani
Jeshi la Polisi viwanja vya ndege linatoa onyo kali kwa abiria wote kufata sheria ikiwemo kuepuka kubeba nyara za serikali pamoja na kutoa ushirikiano.