Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, akizungumza katika kikao chake na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 5, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (kulia) wakiwa katika kikao kikao cha pamoja na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, kilichofanyika jijini Dodoma, Mei 5,2021.
Meneja wa Kampuni ya Equinor Bi. Unni Fjaer, akizungumza katika kikao cha pamoja baina ya Timu ya Serikali ya Majadiliano mradi wa LNG, na kampuni ya Shell, jijini Dodoma, Mei 5, 2021.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt.James Mataragio (kulia), Kaimu Kamishna Msaidizi wa Gesi Bi Joyce Kisamo (Kushoto) wakiwa katika kikao na Waziri wa Nishati na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Eqinor, jijini Dodoma, Mei 5,2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa tatu kushoto)wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa kikao cha Timu ya Serikali ya Majadiliano mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, jijini Dodoma, Mei 5,2021.
Picha mbambali za washiriki wa kikao cha pamoja cha Waziri wa Nishati, na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, jijini Dodoma, Mei 5,2021.
………………………………………………………………………….
Hafsa Omar-Dodoma
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa Serikali inatarajia kuanza majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa kuchataka na kusindika Gesi Asilia (LNG).
Ameyasema hayo, Mei 5, 2021 wakati wa kikao chake na Timu ya Serikali ya Majadiliano ya mradi wa LNG, na kampuni za Shell na Equinor, jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, amesema kuwa, Serikali inataka kuanza utekelezaji wa mradi huo haraka iwezekavyo mara tu baada ya majadiliano kukamilika baina ya Serikali na wawekezaji hao.
Amesema, mradi huo ni muhimu kwa Tanzania, na kwasasa taratibu zote zilizohitajika kufanyika zimekamilika na Serikali ipo tayari kuanza kwa majadiliano hayo ili mradi husika uanze kutekelezwa.
Aidha, amesema lengo la majadiliano hayo ni kuhakikisha kuwa Serikali inapata faida pamoja na wananchi wake na pia makampuni yote ambayo yatawekeza kwenye mradi huo yanapata faida.
Ameeleza kuwa, Serikali imetoa muda wa miezi Sita ili kukamilisha majadiliano hayo, ili kuweza kuingia katika hatua ya pili ya utekelezaji wa mradi husika.
Dkt. Kalemani, ameelekeza kuanza mara moja kwa kazi ambazo hazitahitaji majadiliano ambapo moja ya kazi hizo ni kuwapa wananchi ufahamu kuhusu mradi husika, ili utakapoanza utekelezaji wa mradi wawe tayari na uelewa.
“Wananchi wajulishwe kuna kitu gani kinaendelea, nini wajibu wao, waelezwe manufaa ya mradi huo, waelezwe wanatakiwa kufanya nini na mipaka yao kwenye maeneo hayo, haya mambo ni lazima yaendelee kuanzia sasa na hayahitaji kumalizika kwa majadiliano kwanza.” Alisema Dkt. Kalemani.
Pia, Waziri Kalemani amezitaka timu zote mbili kujipanga na kutochelewesha majadiliano hayo kwakuwa nchi inahitaji mradi huo na Serikali imejipanga kutekeleza kwa kasi kubwa ili ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema kuwa Serikali imetoa muda wa kutosha wa utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wale wote ambao wapo kwenye timu hiyo kufanya kazi kwa juhudi ili jambo hilo likamilike kwa wakati.
Pia, amesema wataendelea kutoa ushirikiano wa kutosha na kusimamia kikamilifu mradi husika kwa karibu zaidi kwani Watanzania wana matumaini makubwa na mradi.
Naye, Meneja wa kampuni wa Equinor Bi.Unni Fjaer amesema kuwa wapo tayari kukaa pamoja na Serikali ili kuweza kulifanyia kazi suala hilo na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unafanikiwa.