Meneja wa sido mkoani Arusha,akitoa mafunzo hayo kwa wataalamu kutoka halmashauri zote mkoani Arusha,(Happy Lazaro)
********************************
Happy Lazaro,Arusha.
Arusha.SHIRIKA la kuhudumia viwanda vidogo nchini, (SIDO),mkoani Arusha, limetoa mafunzo kwa halmashauri zote mkoani hapa juu ya namna ya kuanzisha Kongano za viwanda ili kuongeza ajira na kukuza mnyororo wa thamani kwa bidhaa na mazao ya wakulima.
Meneja wa SIDO mkoani hapa, Nina Nchimbi amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuhamasisha halmashauri hizo ziweze kuanzisha Kongano za viwanda na hivyo kuzalisha ajira zipatazo milioni 8 kwa Watanzania kupitia mpango huo wa kuongeza thamani ya mazao.
Mafunzo hayo yamewashirikisha maafisa biashara, kilimo, ushirika na mipango kutoka halmashauri zote Mkoa wa Arusha.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na shirika la kimataifa la maendeleo ya Japan, (JICA), Sido na ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Arusha.
Nchimbi amesema mpango kama huo umeonyesha mafanikio makubwa kwenye nchi za Sweden, Vietnam na Australia.
Aliongeza kuwa,kwa hapa nchini Kongano zilizoanzishwa na kutoa mafanikio makubwa kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Mtiko Singida, Mpunga Ubaruku mbeya, Mchikichi Kigoma, Mchele Mbeya pamoja na kuziboresha Kongano bubu ili zilete mafanikio .
Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha, (RAS), Hargeney Chitukuro amezitaka halmashauri zote mkoani hapa kuwa tayari kutenga maeneo ya kuanzisha Kongano hizo za viwanda ili bidhaa zitakazozalishwa ziweze kupata soko kwa urahisi na kuboresha bidhaa za uzalishaji.
Chitukuro ambaye ni RAS Msaidizi ,huduma za kiuchumi na uzalishaji Mali mkaoni hapa amesema uanzishaji wa Kongano hizo utasaidia sana kukuza biashara ya wananchi hivyo kuinua uchumi wa mkoa na Taifa.
Mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo, Afisa biashara wa halmashauri ya jiji la Arusha, Privanus Katinhila
amesema uanzishaji wa Kongano za viwanda utakwenda kujibu Kero za wafanyabiashara kwa kuwaunganisha pamoja katika uanzishaji wa viwanda.
“Sekta binafsi kupitia Kongano za viwanda zinaenda kuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kutengeneza ajira kwa vijana,” alisema Katinhila.