Wataalamu wabobezi wa moyo na wazibuaji wa mishipa ya damu ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri wakimtibu mgonjwa mwenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambaye mapigo yake ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s) wakati wa kambi maalum siku mbili ya matibabu hayo iliyofanyika hivi karibuni katika Taasisi hiyo. Jumla ya wagonjwa sita walitibiwa katika kambi hiyo.
Picha na JKCI
………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Wagonjwa sita wenye matatizo ya hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yao ya moyo yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s) wamepata matibabu katika kambi maalum ya matibabu hayo iliyomalizika hivi karibuni katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo ya siku mbili ilifanywa na madaktari wa Taasisi hiyo kwa kushirikiana na wenzao kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mtaalamu mbobezi wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambaye pia ni mratibu wa kambi hiyo Dkt. Yona Gandye alisema katika hali ya kawaida moyo hupiga kati ya mapigo 60 hadi 100 kwa dakika.
Dkt. Gandye alisema mtu akiwa na tatizo katika mfumo wa umeme wa moyo ambalo anaweza kulipata aidha kwa kuzaliwa nalo au athali ya ugonjwa linapelekea mfumo wa umeme wa moyo kubadili mapigo yake inaweza kuwa chini ya mapigo 60 kwa dakika au kuwa juu ya 100 kwa dakika.
“Sababu mbalimbali zinaweza kuufanya moyo udunde kwa haraka kuliko kawaida hii ni pamoja na mtu kuzaliwa na tatizo, kwa kurithi kutoka kwa wazazi hata kama wao hawakuwa na dalili. Sababu ya pili ni ugonjwa wa shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na kuwa na misuli mikubwa ya moyo (Hypertrophy).
“Mgonjwa anakuja kliniki akiwa na dalili za moyo kushindwa kufanya kazi ambazo ni miguu kuvimba, pumzi kubana, kushindwa kulala vizuri usiku. Ukimfanyia vipimo unakuta moyo wake umetanuka na umefika mahali umeme wake wa moyo haufanyi kazi vizuri”, alisema Dkt. Gandye.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo na matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo Prof. Mervat Aboulmaaty kutoka Hospitali ya Shifa iliyopo nchini Misri alisema amefurahi kuona taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imefunga mtambo wa kisasa wa Cathlab ambao umeungaishwa na mtambo wa Carto 3 System 3D & mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Prof. Mervat alisema, “Kufungwa kwa mashine hii ya kisasa na yenye teknlologia ya hali ya juu kutaweza kuokoa maisha ya watu wengi wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo nchini Tanzania”,.
Alisema katika katika kambi hiyo licha ya kutibu, wataalamu walibadilishana ujuzi wa jinsi ya kutibu wagonjwa wenye tatizo hilo la moyo unaokwenda kwa haraka.
Aliongeza kuwa kupitia chuo kikuu cha Ain Shams cha nchini Misri wanatoa elimu kwa njia ya mtandao kuhusu matibabu hayo ambapo madaktari wengi wa Afrika wakiwemo wa Tanzania wamekuwa wakishiriki.
“Hii inamaana kuwa baada ya miaka michache ijayo tutakuwa na madaktari wengi wenye utaalamu wa kutoa matibabu ya hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda haraka kuliko kawaida na kuweza kuokoa maisha ya wagonjwa wenye matatizo haya”, alisema Prof. Shams ambaye pia ni mkufunzi katika chuo hicho.
Naye mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Reuben Mutagaiwa ambaye alishiriki katika kambi hiyo alisema waliandaa wagonjwa ambao walikuwa na dalili za ugonjwa wa mfumo wa umeme wa moyo baada ya kuwachunguza kwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Stress Electrocardiography – ECG) waligundulika kuwa na tatizo.
“Ili kuchunguza na kubaini zaidi kuna vipimo ambavyo vinafanyika kwa kitaalamu vinajulikana kama Electrophysiological (EP) studies & ablation ambapo mgonjwa anaingizwa katika chumba cha upasuaji (Cathlab) kwa ajili ya uchunguzi wa mfumo wa umeme wa moyo (electrophysiology) unasisimua yale matatizo ambayo yalionekana katika kipimo cha ECG (Induction of Arrhythmias) baada ya kuuleta umeme wa moyo ambao hauna upangilio unaweza kufahamu ni upande gani umeme huo unatoka na kuweza kuudhibiti”, alisema Dkt.Mutagaiwa.
Dkt. Mutagaiwa alisema baada ya kugundua kama tatizo liko kwenye upande wa kushoto au wa kulia wa moyo kuna kifaa maalum kiitwacho Ablator ambacho kinatoa joto na ukiliweka sehemu ambayo umeme wa moyo hauna mpangilio unatoka unaweza kumtibu mgonjwa kwa kuziunguza njia hizo.
“Kwa kawaida wagonjwa hawa walikuwa wanawekwa katika dawa za vidonge lakini dawa zinaukomo wake, hadi wanafanyiwa matibabu haya walishashindikana kwenye dawa hivyo basi matumizi ya dawa tuliyasimamisha na kuwafanyia tiba hii”.
“Faida kubwa ya tiba hii ni mgonjwa kupona moja kwa moja na baadaye mgonjwa anashauriwa kutumia dawa na kuendelea na kliniki yake kama kawaida”, alisisitiza Dkt. Mutagaiwa.
Matibabu hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza katika maabara ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo (Catheterization Laboratory – Cathlab) mpya ambapo mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kufunga mtambo huo ambao umeungaishwa na mtambo wa Carto 3 System 3D & mapping electrophysiology System wenye uwezo wa kufanya uchunguzi na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Matibabu ya tatizo la hitilamu ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yake yanakwenda haraka kuliko kawaida (Tachyarrhythmia’s) yalianza kutolewa hapa nchini mwaka 2019 ambapo hadi sasa wagonjwa 11 wameshapata matibabu.