Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ndege Tanzania(ATCL) Injinia Ladslaus Matindi akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu wa shirika hilo mtaa wa Ohio jijini Dr es salaam wakati akitangaza kuanza tena kwa safari za ndege hiyo kwenda nchini China Mei 8,2021.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ndege Tanzania(ATCL) Injinia Ladslaus Matindi wakati akizungumza nao leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ndege Tanzania(ATCL) Injinia Ladslaus Matindi wakati akizungumza nao leo jijini Dar es salaam.
…………………………………..
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ndege Tanzania(ATCL) Injinia Ladslaus Matindi amesema kampuni hiyo inatarajia kuanza rasmi safari zake mwishoni mwa wiki hii kwenda mji wa Guangzhou nchini China na hiyo ni baada ya kupewa vibali na Serikali ya nchi hiyo kwa ajili ya kuanza kufanya safari hiyo.
Mkurugenzi huyo ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya kampuni hiyo mtaa wa Ohio jijini Dar es Salaam
Amesema kuanza kwa safari hizo kunatokana na kufikiwa kwa makubaliano mbalimbali baina ya China na shirika hilo hususani juu ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid -19.
Ameongeza kuwa safari ya ndege hiyo inayotarajiwa kufanyika mara moja kila baada ya wiki mbili au mara mbili kwa mwezi, inatarajiwa kuwahusisha raia wa China na wale wenye vibali maalumu vya kuishi nchini humo kwa safari za kwenda na kwa safari za kurudi nchini abiria yoyote ataruhusiwa kuja na ndege hiyo.
Aidha amesema ili abiria aweze kusafiri na ndege hiyo itakayotumia wastani wa saa 14 kutoka Dar es Salaam hadi nchini humo, atalazimika kufanyiwa vipimo vitatu vya Covid 19 siku tatu mfululizo kabla ya safari huku siku ya safari akifanyiwa kipimo kingine cha haraka na kuruhusiwa kupanda ndege.
“Tunaishukuru Serikali yetu iliwezesha kupatikana kwa kipimo hicho cha IGM ambapo pamoja na kipimo kijulikanacho kama PCR itamlazimu kila msafiri kufanyiwa ili kujiridhisha kama hana Corona ndipo aweze kusafiri” amesema Matindi.
Kuhusu safari Mkurugenzi huyo mtendaji wa ATCL alisema matarajio yao ndege hiyo itakuwa ikifanya safari zake kila jumamosi saa kuanzia saa 11 alfajiri na kufika saa 3 usiku kisha kuanza safari saa 5 usiku wa siku hiyo hiyo kutoka China na kuwasili hapa nchini Jumapili saa 5 asubuhi.
Amesema kwa wasafiri wanaotarajiwa kusafiri na shirika hilo kwenda China, watalazimika kukata tiketi ya safari hiyo kupitia mawakala watatu waliopewa jukumu hilo na ATCL ambayo majina ya mawakala hao yanapatikana katika tovuti ya shirika hilo.