*******************************
NA NAMNYAK KIVUYO,ARUSHA.
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo amesema kuwa Shule ya St Jude inatakiwa kuungwa mkono kutokana na kazi wanayoifanya ya kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata elimu bure jambo ambalo sehemu ya utelelezaji wa sera ya serikali ya elimu bure ambayo walishaanza kuitekeleza muda mrefu na kwa upana zaidi.
Gambo aliyasema hayo baada ya kuitembelea shule hiyo ili kujiridhisha kutokana na changamoto zilizoibuka hivi karibuni za akaunti za banki kufungwa na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na kuchukua shilingi milioni 500 zilizokuwepo kwenye akaunti hiyo.
Gambo alisema kuwa ametembelea, amekagua na ameeleweshwa juu ya upatikanaji wa wanafunzi wa shule hiyo ambapo mchakato mzima unashirikisha serikali kwa asilimia 100 kuweza kuwapata watoto wenye chagamoto kweli, jambo ambalo ni jema kwani ufadhili unawafikia watoto husika na ni bure na sio kama baadhi ya watu wanavyosema.
“Fedha hizo zilizochukuliwa nimeambiwa zilikuwa za mahitaji ya shule ikiwemo mishara ya wafanyakazi, chakula na malazi mengine ya wanafunzi hawa jambo ambalo nimeshaongea na waziri mwenye dhamana na ameniahidi atalishughulikia ili muweze kuendelea na kazi yenu hii ya kuisaidia serikali kutoa elimu bure ma hamfanyi biashara sasa mkiambiwa mlipe kodi fedha hizo zitatoka wapi?,”Alieleza Gambo.
Alifafanua kuwa katika suala la vibali vya kazi kwa wafanyakazi wakigeni wawili hilo nalo atazungumza na wanaohusika ili kuangalia ni namna gani wanawasaidia kuendelea kufanya kazi kwa amani ambapo shule hiyo ina wafanyakazi 302, mia mbili tisini na saba wakiwa ni watanzania sawa na asilimia 97, huku watano wakiwa nia wageni sawa na asilimia 3 jambo ambalo endapo shule hiyo itafungwa watakaoumia ni wazawa.
Alisema kuwa shule hiyo haijiendeshi kibiashara ambapo ina wanafunzi zaidi ya 1800 huku 437 wakiwa ni wa shule ya msingi, sekondari ya wasichana yenye mchepuo wa sayansi 428 na waliobaki wakiwa ni wanafunzi wa shule mchanganyiko iliyopo usariver ambao ni kwanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha sita huku wote wakipata elimu kwa ufadhili wa watu wa Australia.
“Serikali yetu inatoa elimu bure kwanzia chekechea hadi kidato cha nne lakini tunawaona hawa wanatoa bure hadi kidato cha sita kwakeli serikali inatakiwa kuwaangali na kuweza kuwaondolea hizi changamoto kwani tunatamani shule hii ikue na kuenea Tanzania bara yote na kufika Tanzania visiwani pia, kwani hata kule kuna watoto wanaoishi katika mazingira magumu,”Alisema Gambo.
“Kazi wanayoifanya St Jude ni kazi ya Mungu na sio ya kidunia na wanaishirikisha serikali kwa asilimia 100, wamekubali kutoka kwenye nchi zao na kuja kuweka alama ya kuondoa umasikini Tanzania kwa kuwafadhili watoto wetu wanaishi katika mazingira magumu kupata elimu ya msingi hadi sekondari ya juu bure, watu kama hawa wanatakiwa waitwe na kuulizwa wanapokwama na kusaidiwa ili waweze kuendelee kuzalisha matunda katika nchi yetu,”Alisisitiza Gambo.
Kwa upande wao kiongozi wa wanafunzi upande wa shule ya msingi Johnson Eliasafu alisema kuwa ziara hiyo imekuwa taa ya matumaini ya uhusiano mzuri kati yao, jamii na serikali kwa ujumla ili kuweza kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.
Aidha alieleza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali,wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakishiriki maonyesho ya ugunduzi wa kusayansi ambayo hufanyika kila mwaka katika shule ya sekondari ya St.Jude ambapo miradi yao imekuwa ikipata alama nzuri ikiwa ni uungaji mkono juhudi za serikali za kuzalisha wataalamu wa masuala ya kisayansi.
Naye Dada mkuu wa shule ya sekondari ya wasichana iliyojikita kufundisha masomo ya sayansi Vivian Gasper alisema kuwa wanawezeshwa na wahisani wanaogharamia gharama zao zote kwa asilimia 100 na wanategemea baada ya kumaliza masomo wataenda kuwa msaada kwa familoa zao, jamii na taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Bibiana Mardai alisema kuwa wanaiomba serikali iangalie shule hiyo kwa jicho la pili kwani wanawasaidia watoto wa Kitanzania ambao pengine wangeshindwa kusoma kutoka kana na hali duni za familia zao kuweza kufikia maono ya na ndoto zao kwa kupata elimu ambayo itawasaidia kuja kuzitumikia jamii zao hapo baada.
“Hawa ndio viongozi wa kesho huwenda Rais mama Samia mwingine akaja kutokea huku, ni viongozi na ni watu ambao tunatarajia wataleta mapinduzi ya kimaendeleo baadae katika jamii,”Alisema Bibiana.