Home Mchanganyiko MHE. RAIS ATATUA CHANGAMOTO NYINGI ZA WATUMISHI KUPITIA VIPAUMBELE ALIVYOVITOA MEI MOSI-...

MHE. RAIS ATATUA CHANGAMOTO NYINGI ZA WATUMISHI KUPITIA VIPAUMBELE ALIVYOVITOA MEI MOSI- Mhe. Mchengerwa

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watumishi wa Mkoa wa Mwanza leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella.

Baadhi ya Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Mwanza wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa kuzungumza na Watumishi wa Mkoa wa Mwanza leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao.

Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bibi Hosiana Kusiga akiwasilisha hoja ya kiutumishi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Waziri huyo ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akijibu hoja za kiutumishi za Watumishi wa Umma Mkoa wa Mwanza leo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo. Kushoto kwake ni Naibu Waziri, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Angelina Mabula.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akifuatilia taarifa ya utekelezaji ya Mkoa wa Mwanza aliwapowasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo leo ili kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella.

*****************************

Na. James K. Mwanamyoto-Mwanza

Tarehe 3 Mei, 2021

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kuzifanyia kazi changamoto za kiutumishi zinazowakabili Watumishi wa Umma kwa muda mrefu ili waweze kutoa huduma bora kwa umma.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Mwanza leo, Mhe. Mchengerwa amesema hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wakati wa Sherehe za Mei Mosi, 2021 imeainisha wazi azma yake ya kuzifanyia kazi changamoto za Watumishi wa Umma nchini.

Mhe. Mchengerwa, amesema hotuba ya Mhe. Rais ni sehemu ya mijadala inayohusu haki na stahili za Watumishi wa Umma nchini, hivyo hatuna budi kumpongeza kwa kuliona hili na kulitolea maelekezo, na kuongeza kuwa Watendaji na Maafisa Utumishi watekeleze kikamilifu maelekezo hayo ili kuondoa changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma.

Ili kuunga mkono azma ya Mhe. Rais, Mhe. Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu kwani Serikali ya Awamu ya Sita tangu iingie madarakani ikiwa ni kipindi cha miezi miwili tu imedhamiria kuondoa kabisa changamoto zinazowakabili watumishi ili kuwajengea ari kiutendaji.

Akitolea ufafanuzi wa baadhi ya vipaumbele katika hotuba hiyo, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza Watendaji na Maafisa Utumishi kutoa elimu kwa Watumishi walio chini yao juu ya vipaumbele hivyo ili Watumishi hao wapate kuelewa kwa ufasaha namna Serikali ilivyowaondolea changamoto zilizokuwa zikiwakabili.

Akitolea mfano wa kipaumbele cha punguzo la asilimia moja (1%) ya makato kulingana na stahiki anayopata Mtumishi wa Umma (PAYE), Mhe. Mchengerwa amesema, Mhe. Rais amewapunguzia mzigo mkubwa Watumishi wa Umma katika hili na kutolea mfano kuwa mtumishi anayepokea mshahara wa shilingi laki 3, punguzo la kodi yake ni ni shilingi 30,000 ambayo ni sawa na kumuongezea Mtumishi wa Umma nyongeza ya mshahara wa shilingi 30,000.

“Natamani sana elimu itolewe kwa Watumishi juu ya punguzo hili, ili waone ni kwa kiasi gani Mhe. Rais alivyo na mapenzi mema kwa Watumishi wa Umma.” Mhe. Mchengerwa ameongeza.

Pia amewataka Watendaji katika Taasisi za Umma kutoa ufafanuzi wa vipaumbele vingine vinavyohusu stahiki za Watumishi wa Umma vilivyoainishwa kwenye hotuba ya Mhe. Rais ikiwemo suala la punguzo la asilimia 6 ya makato ya Bodi ya Elimu ya Juu na kuongezeka kwa ukomo wa umri wa watoto kutoka miaka 18-21 kwenye huduma ya Bima ya Afya.

Akizungumzia suala la upandishwaji wa madaraja, malimbikizo ya madai ya Watumishi, maboresho ya miundo ya kiutumishi kwa baadhi ya kada na ajira mpya, Mhe. Mchengerwa amesema, katika kutekeleza vipaumbele vya Mhe. Rais, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kulipa madai ya watumishi, bilioni 499 kwa ajili ya upandishwaji wa madaraja, bilioni 120 kwa ajili ya kuboresha miundo ya baadhi ya kada na zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kuajiri Watumishi 40,000 katika sekta ya Afya, Elimu, Ardhi na Kilimo.

Amewasisitiza Watendaji na Maafisa Utumishi kuzifanyia kazi changamoto za kiutumishi wa watumishi walio chini yao, ikiwa ni pamoja na kuwasilisha madai ya watumishi ili yaweze kuhakikiwa na kulipwa.

Aidha, Mhe Mchengerwa amesisitiza kushughulikia kwa wakati mashauri ya kinidhamu ya Watumishi wa Umma ili kuindolea Serikali mzigo wa kulipa fidia pindi Watumishi hao wanapokata rufaa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi na kushinda rufaa zao.

Kuhusiana na mafunzo kwa Viongozi na Watumishi wa Umma, Mhe. Mchengerwa amehimiza Waajiri kuhakikisha wanawapeleka Watumishi kupata mafunzo katika Chuo cha Utumishi wa Umma na Viongozi kushiriki mafunzo ya namna bora ya uongozi katika Taasisi ya Uongozi.

Kuhusu mafao ya Wastaafu, Mhe. Mchengerwa, amewataka Waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya Watumishi wa Umma kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa wakati ili wanapostaafu waweze kupata stahiki zao kwa wakati.

Ziara ya Mhe. Mchengerwa imelenga kutoa ufafanuzi wa vipaumbele katika hotuba ya Mhe. Rais aliyoitoa wakati wa Mei Mosi, 2021 na kuhimiza utekelezaji wa vipaumbele hivyo kwa Watendaji ili kuwawezesha Watumishi wa Umma kupata stahiki zao mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.