Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam.
PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO
***************************
NA EMMANUEL MBATILO
Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini imefanikiwa kuwakamata watuhumiwa saba na dawa za kulevya kiasi cha kilo 859.08 za aina mbili tofauti ambazo zimekamatwa katika bahari ya hindi zikiwa zinasafirishwa na raia wa Iran.
Akitoa taarifa hiyo leo mbele ya waandishi wa habari mapema Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo Gerald Kusaya alisema kwamba kati ya kilo hizo 355 ni Heroin Hydrochloride na kilo 504.36 ni Methamphetamine ambazo zilikua zimefichwa ndani ya Jahazi la uvuvi lililokua likitokea Irani.
Alisema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ kamandi ya Wanamaji pamoja wamefanikiwa kuwakamata raia hao wa Irani ambapo mpaka sasa mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Vyombo vya usalama wanaendelea na upelelezi kujua ni wapi walipokua wanapeleka Dawa hizo.
Kamishna Kusaya aliwataja watuhumiwa hao kua ni Jan Mohamed Miran(42)ambaye ni nahodha wa jahazi hilo , Amir Huessein Kasom (35) , Issah Baluchi Ahmad (30) Salim Baluch Fedhmuhammad (20), Ikbal Pakil Mohammad (22) Jawid Nuhan NurMohammad (19) pamoja Mustaphar Nowan Kadirbaksh (20).
” Ukamataji huu ni mkubwa kuwahi kufanyika Nchini tangu kuanzishwa kwa Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na Dawa za kulevya mwezi februari 2017 mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Maria Bantulayne na kusomewa mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya ” alisema.
Aliendelea kufafanua kuwa Matumizi ya dawa za kulevya husababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo ya akili, uraibu, moyo, Ini na mapafu pamoja na kuchangia kuenea kwa maambukizi ya Vvu , Virusi vya homa ya ini na kifua kikuu kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.
“Mapambano sasa yanaanza mamlaka hatutalala tutafanya kazi kwa ukamilifu kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na tutawashirikisha watanzania , hivi vita kazima tutashinda na tutafanya shughuli hii usiki na mchana hatutachoka” alisisitiza Kamishna Kusaya.