Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazurui akitoa tamko kwa wamiliki wa Hospitali binafsi kukamilisha taratibu za kisheria za kufanya shughuli zao za kutoa .
************************
Na Ramadhani Ali – Maelezo 30.04.2021
WIZARA ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto imetoa muda wa wiki moja, kwa vituo vya Afya binafsi 12 ambavyo vimeshindwa kukamilisha taratibu za kisheria za usajili kwenda kukamilisha na watakaoshindwa vituo vyao vitafungiwa .
Akizungumza na baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo Ofisini kwake Mnazimmoja, Waziri wa Wizara hiyo Nassor Ahmed Mazurui amesema Serikali haipendi kuvifungia vituo vya Afya lakini sheria za nchi laima zifuatwe.
Amesema Hospitali na Vituo vya afya binafsi ni mdau na inathamini mchango mkubwa wanaotoa katika kuimarisha huduma za afya, na Serikali itaendelea kutoa kila msaada kuhakikisha wanatowa huduma bora kwa wananchi..
Waziri Mazurui amewataka wamiliki wa vituo vya Afya binafsi kuendeleza mashirikiano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na watakapohisi kuna sheria kandamizi wasisite kutoa mapendekezo kwa Wizara na ameahidi yatafanyiwa kazi.
Msaidizi Mrajisi wa Bodi ya ushauri ya Hospitali binafsi Khamis Makame Haji amesema wamiliki wa Hospitali walitakiwa kukamilisha taratibu za usajili mpya kwa mwaka 2021 mpaka kufikia Januari 15 lakini kutokana na matatizo yaliyojitokeza waliongeza muda mpaka mwezi Machi na baadhi walishindwa kufanya usajili huo.
Amesema Bodi ya ushauri ilifanya juhudi kubwa ya kuwafuatilia na kuwahimiza wamiliki hao ili waweze kuendeleza shughuli zao hata hivyo wengine walipuuza.
Baadhi ya wamiliki waliotakiwa kukamilisha taratibu za usajili mpya 2021 wameahidi kuwa katika kipindi hicho cha wiki moja watahakikisha wanatekeleza agizo walilopewa na Waziri.
Vituo vya afya vilivyotakiwa kurekebisha kasoro zao ni Utapoa cha Mfenesini, Imani Kliniki ya Mwembemimba, Mahonda Kliniki ya Mahonda, Ahsana ya Nungwi, Maungani Kliniki ya Maungani, na Mustafa Unali ya Kisauni,
Nyengine ni Nyango Dispensari ya Kisauni, Maryam Kliniki ya Mwanakwerekwe, Tourism Medical Servise ya Paje, Hekima Medical Kliniki ya Kwamchina mwanzo, Zamzam Dispensary ya Bububu na Furaha Dispensary ya Kianga.
Wakati huo huo Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Nassor Ahmed Mazurui amepokea msaada wa dawa kutoka Kampuni ya Wide Spectrum Limited ya Dar es salaam kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Zanzibar.
Meneja Masoko wa Kampuni ya Wide Spectrum Khamis Saleh Fakir alimkabidhi Waziri Mazurui msaada huo na kusema ni sadaka yao kwa wananchi katika kipindi hichi cha mwezi wa Ramadhani.
Amesema Kampuni yao ni wadau wakubwa wa afya na wiki iliyopita walikuwa Pemba na walitoa msaada wa dawa Hospitali ya Wete na Chake chake na wataendelea kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar kusaidia hospitali na vituo vya afya,
Waziri Mazurui alimshukuru Meneja Masoko wa Kampuni ya Wide Spectrum kwa msaada wa dawa na kumueleza kuwa Wizara inathamini watu wenye moya wa kusaidia wananchi wenzao.