Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Fadhili Manongi akizungumza wakati wa ziara katika Mamlaka ya maji na usafi wa mazingira DUWASA mara baada ya kutembelea maeneo ya Chamwino linapojengwa tanki kubwa la maji na eneo ya Ihumwa kunakochimbwa visima.
Kaimu Mkurugenzi wa EWURA Mhandisi Godfrey Chibulunje akizungumza wakati wa ziara ya bodi ya EWURA walipotembelea miradi ya maji ya DUWASA kuona utekelezaji wake.
Kaimu Mkurugenzi wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph akizungumza wakati wa ziara ya bodi ya EWURA na watumishi wa EWURA walipotembelea miradi ya Mamlaka hiyo kuona utekelezaji wake katika kumaliza tatizo la maji Jijini Dodoma.
Makamu Mwenyekiti wa bodi ya DUWASA bi Neema Majule akizungumza wakati wa ziara ya Bodi ya EWURA na watumishi wa EWURA walipotembelea miradi ya Mamlaka hiyo kuona utekelezaji wake katika kumaliza tatizo la maji Jijini Dodoma.
Meneja wa ufundi wa DUWASA Mhandisi Kashilima Mayunga akitoa taarifa wakati wa ziara ya bodi ya EWURA na watumishi wa EWURA walipotembelea miradi ya Mamlaka hiyo kuona utekelezaji wake katika kumaliza tatizo la maji Jijini Dodoma.
……………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Bodi ya Mamlaka ya udhibiti wa Nishati na Maji EWURA imeitaka Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira Mkoa wa Dodoma DUWASA kuhakikisha wanadhibiti upotevu wa maji sambamba na kutoa taarifa kwa wakati kwa wananchi pindi inapotokea kukosekana kwa huduma hiyo.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya EWURA Fadhili Manongi wakati bodi hiyo ilipotembelea DUWASA na kuongea na bodi ya DUWASA na watumishi kwa lengo la kupata taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji na mipango ya baadaye kumaliza tatizo la maji.
Amesema licha ya mipango mizuri inayofanywa na DUWASA katika kuhakikisha tatizo la maji linamalizika Jijini Dodoma lakini wahakikishe taarifa sahihi zinawafikia wananchi kwa wakati pindi huduma hiyo inapokuwa na hitilafu.
“Tumesikia mipango yenu kwa kweli ni mizuri na imelenga kumaliza kero ya maji lakini kuna kipindi huduma ya maji inapokosekana taarifa hazifiki kwa wananchi na kupelekea wananchi kulalamika” amesema Manongi.
Pia ameitaka DUWASA kuhakikisha inadhibiti upotevu wa maji katika maeneo mbalimbali kwamba kitendo hicho kinapelekea baadhi ya maeneo kukosa huduma za maji, wakati maji yanayopotea yangedhibitiwa ingesaidia kupunguza uhaba wa maji.
Ameitaka Mamlaka hiyo kushirikiana na Wizara ya maji kuhakikisha malengo ya muda mrefu ya kusogeza huduma ya maji kutoka ziwa Victoria na kutoka bwawa la Fwarukwa inatiliwa mkazo ili kuhakikisha huduma ya maji inazidi kuboreka katika jiji la Dodoma.
Amesema kuna haja ya kufanyika kwa jitihada za kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dodoma kwa kuwa kwa sasa kunaongezeko kubwa la watu kuhamia Dodoma mara baada ya Serikali kuhamishia makao makuu Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa bodi ya EWURA wamepongeza jitihada kubwa zilizofanywa na DUWASA kuwa katika ziara yao ya kwanza kulikuwa na changamoto nyingi na maswali yaliyokuwa hayajibiki lakini kwa sasa jitihada zimeonekana na kuonyesha mwanga wa kumaliza tatizo la maji Dodoma.
“Ziara ya kwanza tulikuwa na maswali mengi kuliko majibu lakini kwa sasa kuna unafuu majibu yanajitosheleza na sisi sasa tunapata confidence (ujasili) kuwa tatizo litakwisha, hasa kwa sababu Dodoma ni ajenda yetu ya kudumu kuhakikisha tatizo la maji linakwisha” amesema Richard Kayombo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Mhandisi Godfrey Chibulunje ameishukuru Bodi hiyo kwa kuridhika na utoaji huduma na mipango ya DUWASA huku akiitaka DUWASA kuongeza bidii katika kutatua tatizo la maji katika jiji la Dodoma na Mkoa kwa ujumla.
Nae Kaimu Meneja wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema amesema Jiji la Dodoma linaupungufu wa maji takribani lita elfu thelathini na saba (37,000) kwa siku, na maji yanayozalishwa kwa sasa kwa vyanzo vyao vyote ni elfu sitini na sita na mia sita(66,600) kwa siku huku mahitaji ni lita laki moja na tatu na mia sita(103,600) kwa siku.
Amesema katika kukabiliana na upungufu huo wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwamo kuchimba visima pembezoni mwa mji ili kuongeza upatikanaji wa maji katika jiji la Dodoma.
Pia amebainisha kuwa wamekuwa wakifanyakazi kwa ukaribu na EWURA na wamekuwa wakiwakumbusha mara kwa mara namna ya kutoa huduma kwa wateja wao kuhusu upotevu wa maji amesema wamekutana na watendaji wa kata na wenye viti wa mitaa yote ili kusaidia kutoa taarifa ya upotevu wa maji na vitendo vya wizi wa maji.