Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Charles Meshack akizunguza katika kikao maalum cha wadau kupanga mikakati ya uhifadhi wa Misuti kilichofanyika kwenye hoteli ya Morena jijini Dodoma.
Charles Leonard Meneja Mradi wa TFCG akichangia jambo katika kikao hicho kilichofanyika kwenye hoteli ya Morena jijini Dodoma.
John Yonazi Mwenyekiti wa Bodi ya TFCG akifunga kikao hicho mara baada ya kumaliza majadiliano yake kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa utunzaji wa misitu.
John Yonazi Mwenyekiti wa Bodi ya TFCG akijadiliana jambo na Ofisa Mawasiliano wa TFCG, Bettie Luwuge mara baada ya kikao hicho kumalizika.
Ofisa Mawasiliano wa TFCG, Bettie Luwuge akifafanua jambo katika kikao hicho.
Baadhi ya wadau kutoka Taasisi mbalimbali za utunzaji wa misitu wakiwa katika kikao hicho.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Lucas Lemomo akichangia hoja katika kikao hicho.
Picha ya pamoja.
……………………………………….
NA SULEIMAN MSUYA, DODOMA
IWAPO dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ), haitasambazwa kwenye vijiji vyenye misitu upo uwezekano wa hekta milioni 17 za misitu kupotea ifikapo 2070.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG), Charles Meshack wakati akizungumza na wadau mbalimbali kutoka Serikali na sekta binafsi wanaohusika na sekta ya misitu waliokutana jijini Dodoma.
Meshack amesema Tanzania ina hekta za misitu milioni 48.1 ambapo hekta milioni 22 ni misitu ya vijiji hivyo USMJ ndio njia pekee inaweza kuinusuru isiishe.
Amesema hadi sasa USMJ ipo kwenye hekta milioni 5 pekee kati ya hekta milioni 22 iliyopo kwenye vijiji hali ambayo ni hatari katika rasilimali hiyo.
Meshack amesema hofu ya kumalizika kwa misitu inaongezeka zaidi baada ya kuja kwa GN 417 ambayo inaonekana kufanya kazi kwenye misitu iliyopo kwenye USMJ pekee jambo ambalo limeanza kukatisha tamaa wanavijiji.
Amesema takwimu zinaonesha kwa mwaka zaidi ya hekta 469,000 za misitu zinapotea nchini hivyo Serikali inapaswa kuangalia upya GN 417 ili iweze kukidhi haja ya kuendeleza rasilimali misitu.
“Ujio wa GN 417 umezidisha hofu na kukatisha tamaa wanavijiji ambao wapo kwenye USMJ kwani kwa sasa mazao ya misitu hayatoki kwani misitu isiyo na USMJ takribani hekta milioni 17 uvunaji wake hauna mazingira magumu,” amesema.
Amesema kumekuwepo na kasi kubwa ya uvunaji mazao ya misitu kama mkaa na mbao kwenye maeneo ambayo hayana USMJ na msukumo mkubwa ni kutotumika GN 417 kwenye maeneo hayo.
“Hali inaonesha kuwa kama hakutakuwa na USMJ miaka 50 ijayo misitu itakuwa imeisha na sababu kubwa ni kilimo na ufugaji ambavyo kwa upande fulani vinaonekana kuchochea maendeleo,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema zipo changamoto za kiutendaji na kisera ambazo msingi mkubwa ni kuongeza uzalishilaji kwa sekta husika.
“Hizi changamoto zinaweza kupata muafaka kwa wadau kujadiliana na kuwa na kauli moja ambayo kila sekta itazingatia eneo lake na sio kushindana.
Lakini pia changamoto ya GN 417 inapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma ili kutokatisha tamaa vijiji vinavyotekeleza USMJ,” amesema.
Meshack amesema changamoto nyingine ni misitu ya asili kutopewa kipaumbele kama isiyo ya asili jambo ambalo linaondoa ari ya uhifadhi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Morogoro, Lucas Lemomo amesema USMJ umechangia mafanikio mengi katika vijiji vitano vilivyopo kwenye halmashauri yake hivyo ni jambo la kuungwa mkono.
Lemomo ambaye ni Diwani wa Kata ya Matuli amesema kumekuwepo na changamoto kutoka Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) kushindwa kutoa vibali vya kusafirisha mazao ya misitu kwa haraka.
“Lakini katika hali ya kushangaza TFS haohao wanatoa vibali kwa haraka kwa wafanyabiashara wanaonunua nje ya maeneo yenye USMJ hali ambayo inakatisha tamaa,” amesema.
Diwani wa Kata ya Kisanga Halmashauri ya Kilosa mkoani Morogoro, Hassan Kambenga amesema wilaya hiyo ina vijiji 20 vinavyotekeleza USMJ na asilimia kubwa wananchi wamenufaika kwa huduma nyingi.
Amesema Serikali inapaswa kutenga bajeti kuhakikisha kuwa USMJ inasambaa kila kona ya nchi kwa kuwa ina faida na kuachana na kuja na sheria zenye kukwamisha mafanikio hayo.
“Hili la wavunaji wa mazao ya misitu waliopo kwenye USMJ kutohudumiwa na TFS vizuri lipo hadi Kilosa hivyo tunaomba wabadilike kwani wanatoa tafsiri mbaya,” amesema.
Naye mnufaika wa dhana ya USMJ, Kulangwa Ganda kutoka Kijiji cha Kitunduweta Wilayani Kilosa amesema wamenufaika hivyo kuitaka serikali iendeleze dhana hiyo.
“Niombe Serikali isiwe sehemu ya kikwazo kwenye miradi hii ya USMJ kwani ina matokeo chanya yanayopaswa kuendelezwa,” amesema.