Mkuu wa Atomiki Kanda ya Mashariki, Dkt.Wilbroad Muhogora akifungua mafunzo ya siku 5 ya kitaifa ya usafirishaji salama wa vifaa vya kinyuklia na vyanzo vya mionzi yanayofanyika kuanzia leo Jijini Dar es Salaam. Wadau mbalimbali wa Atomiki wakifuatilia mafunzo ya siku 5 ya kitaifa ya usafirishaji salama wa vifaa vya kinyuklia na vyanzo vya mionzi yanayofanyika kuanzia leo Jijini Dar es Salaam.Mkuu wa Atomic Kanda ya Mashariki, Dkt.Wilbroad Muhogora akipata picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa Atomiki katika mafunzo ya siku 5 ya kitaifa ya usafirishaji salama wa vifaa vya kinyuklia na vyanzo vya mionzi yaliyofanyika kuanzia leo Jijini Dar es Salaam.
PICHA NA EMMANUEL MBATILO
************************************
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM.
TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), inaendesha mafunzo ya siku Tano (5) ya Kitaifa ya utunzaji na usafirishaji salama wa vyanzo vyenye viasili vya Mionzi (Radioactive source), kwa taasisi mbalimbali zinazojihusisha na usafirishaji wa mionzi nchini.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea Jijini Dar es Salaam, Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Dk. Wilbroad Muhogora, Mkuu wa Kanda ya Mashariki amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu sana kwani yatawasiaidia washiriki kupata ujuzi wa kuhusu utunzaji na usafirishaji bora na salama wa vyanzo vya mionzi.
Dk Muhogora amesema lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo katika menejimenti ya utunzaji na usafirishaji salama wa vyanzo vya mionzi.
“Usafirishaji wa vyanzo hivi unaweza kusababisha madhara iwapo matakwa ya kiulinzi na usalama hayatazingatiwa wakati wa kuvitunza au kuvisafirisha
Kwa hiyo mafunzo haya yatawasaidia kupata uelewa zaidi na kutayarisha mipango ya kinga mionzi wakati wote”. Alisema Dkt. Muhogora.
Kwa upande wa wadau ambao wanapokea mafunzo wamesema mafunzo hayo yanaweza kusaidia kufahamu mazingatio ili wakiwa wanafanya shughuli ya uhifadhi, utumiaji na usafirishaji wa mionzi au vifaa vilivyo na mionzi waweze kuwa salama.
Vifaa vyenye mionzi vinatumika nchini katika sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo afya, kilimo, ufugaji, viwanda, barabara ambapo mpaka sasa sasa jumla ya idadi ya vifaa vitoavyo mionzi nchini ni karibu 900 na kati ya hivyo vyanzo vya mionzi vyenye viasili vya mionzi (radioactive sources) ni 400.
Mafunzo haya yanahudhuriwa na washiriki kutoka katika taasisi mbali mbali zinazojihusisha na usafirishaji wa vyanzo vya mionzi nchini.