Mkurugenzi Mkuu wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA, Rahima Njaidi akihojiwa na waandishi wa habari katika kikao maalum cha wadau kupanga mikakati ya uhifadhi wa Misuti na Mkaa Endelevu.
Katikati ni John Yonazi Mwenyekiti wa Bodi ya TFCG akiwa pamoja na Charles Meshack Mkurugenzi wa TFCG na Ofisa Mawasiliano wa TFCG, Bettie Luwuge wakiwa katika kikao hicho.
Baadhi ya washiriki wa kikao hicho
Picha ya pamoja.
…………………………………………..
NA SULEIMAN MSUYA, DODOMA
MTANDAO wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA), umesema katika kipindi miaka mitano ijayo wataongeza wana mtandao ili kuchochea uhifadhi wa misitu nchini.
Kwa sasa MJUMITA ina wana mtandao takribani 15,000 kwa miaka 20 ya uwepo wake.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa MJUMITA, Rahima Njaidi wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dodoma.
Amesema MJUMITA imeanzishwa mwaka 2000 ambapo wamekuwa wakijihusisha na usimamizi wa misitu wakiamini ni njia sahihi ya kuifanya iwe endelevu.
Njaidi amesema hadi sasa wamefikia vijiji 452 katika mikoa 13 na kuwapatia mafunzo wanavijiji kuhusu dhana ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Jamii (USMJ).
Amesema katika mchakato huo wamekuwa wakipata ushirikiano mzuri kutoka Serikalini kupitia Idara ya Misitu na Nyuki, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na wengine hali ambayo leo umewezesha kupata wana mtandao takribani 15,000.
“Tunajivunia wananchi wanatuelewa na wanajiunga na mtandao hali ambayo inasaidia uhifadhi kuongezeka.
Ila juhudi za MJUMITA zimewezesha kupata tuzo mwaka 2015 ya UNDP, Tuzo ya JIDE kutoka kwa Malkia wa Sweden yote hayo ni ushahidi kuwa tunagusa wananchi kwenye miradi yetu,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema MJUMITA imefanikiwa kuweka hekta milioni 1.8 ya misitu ya asili chini ya usimamizi wa wana vijiji.
“Mafanikio haya yanatusukuma sisi kuongeza vijiji na mikoa mingine hivyo tutatoka vijiji 452 vilivyopo kwani lengo kuu ni misitu ya Tanzania iwe salama,” amesema.
Aidha, wakati umefika kwa Serikali kuacha uzito kwenye kutekeleza Sera, sheria na mipango iliyopangwa inatekelezwa ili kuilinda na kuiendeleza misitu.
Njaidi amesema kwa sasa Tanzania ipo kwenye awamu ya pili ya USMJ ambayo inataka jamii kunufaika na rasilimali misitu hivyo nguvu ielekezwe huko kuchochea uendelevu wa misitu.
Mkurugenzi huyo amesema serikali inatakiwa kutambua lengo la wadau kama MJUMITA na TFCG ni kuchochea maendeleo na huduma za kijamii na sio wao kunufaika.