Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Baraka Kanunga Laizer akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, baada ya kusomwa maazimio ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na kutambua na kuenzi mchango wa hayati John Magufuli, kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Sendeu Laizer Obama, kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Yefred Myenzi na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Zuwena Omary.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Sendeu Laizer Obama akisoma azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan.
Diwani wa Tarafa ya Ruvu Remit, Rehema Laizer akisoma azimio la kutambua na kuenzi mchango wa hayati Dkt John Magufuli kwa Taifa.
………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametoa azimio la kumpongeza Rais wa awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza Taifa na kutambua na kuenzi mchango wa hayati Dkt John Magufuli.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga Laizer akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani amesema wametoa maazimio hayo kwa lengo la kumpongeza Rais Samia na kuenzi mchango wa kulitumikia Taifa wa hayati Dkt Magufuli.
Kanunga amesema wanaimpongeza Serikali kwa kuwa na mfumo mzuri wa kubadilishana madaraka uliowezesha Taifa kupita salama katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati Dkt Magufuli kwa amani na utulivu hadi kuwezesha kupitishwa kwa Rais Samia.
Amesema wanampongeza Rais Samia kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke na kuweka historia ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika uongozi wa Taifa la Tanzania.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Sendeu Laizer Obama, akisoma azimio la kumpongeza Rais Samia amesema wanampongeza Rais Samia kwa kuonyesha ujasiri, umahiri na weledi mkubwa katika kusimamia shughuli zote za mazishi ya hayati Dkt Magufuli na kuongoza watanzania kutoa salamu za mwisho kwenye maeneo mbalimbali na kupokea wageni wa nje ya nchi wakiwemo marais, mawaziri wakuu, mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa.
“Tunampongeza kwa kauli thabiti, msimamo na mwelekeo aliouonyesha kuhusu Serikali ya awamu ya sita kupitia hotuba mbalimbali alizozitoa wakati akiwaapisha viongozi aliowateua na kupitia hotuba ya kihistoria iliyoweka misingi na mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita aliyoitoa Bungeni Aprili 22 mwaka huu,” amesema Sendeu.
Amesema wanampongeza kwa nia yake thabiti aliyoionyesha ya kuliunganisha Taifa na pia msimamo wake wa kulinda maadili ya kitaifa aliyodhihirisha kwa kukemea ushabiki juu ya masuala yanayolipasua Taifa kupitia mitandao ya kijamii, mijadala ya kibunge na kwenye majukwaa mengine ya kupeana taarifa.
Amesema wanaungana na kauli yake thabiti iliyowahakikishia kuwa ana uwezo, uthubutu, ujasiri, umahiri na weledi wa kutosha wa kuliongoza Taifa kwa kuwa amepitia kwenye mikono ya viongozi mahiri waliomtangulia akiwemo hayati Dkt John Magufuli.
Diwani wa Tarafa ya Ruvu Remit, Rehema Laizer akisoma azimio la kutambua na kuenzi mchango wa hayati Dkt Magufuli amesema wanatambua kazi kubwa iliyofanywa naye katika kupanga, kusimamia na kutekeleza sera, mipango na mikakati mbalimbali inayogusa maisha ya wananchi wa Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, miundombinu, nishati na maendeleo ya viwanda.
Laizer amesema hayati Dkt Magufuli alianzisha na kutekeleza sera ya elimu bila malipo kwa ngazi ya elimu ya msingi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne ambayo imepandisha viwango vya uandikishaji wa wanafunzi, mahudhurio, ufaulu na hata udahili katika vyuo vya elimu ya juu.
Amesema amesimamia ukuaji wa sekta za viwanda, madini, utalii, mawasiliano na uchukuzi na kwa namna ya kipekee kujenga ukuta kwa ajili ya kudhibiti utoroshaji wa madini ya Tanzanite kwenye mji wa Mirerani uliopo Wilayani Simanjiro ambao utabaki kuwa alama ya kukumbukwa kwa wananchi wa Simanjiro.
“Amewezesha ujenzi wa miundombinu ya elimu yakiwemo madarasa, mabweni, nyumba za walimu na mabwalo ya chakula, kufufua shirika la ndege ATCL na kununua ndege mpya 11 na kukarabati na kujenga viwanja vya ndege ili kuboresha sekta za usafirishaji na utalii wa ndani na nje ya nchi,” amesema Laizer.
Amesema hayati Dkt Magufuli ametekeleza miradi mikubwa ya maji kwenye ngazi mbalimbali iliyowezesha wananchi kupata maji safi na salama na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji kwa ajili ya matumizi ya binadamu na mifugo ukiwemo mradi mkubwa wa maji wa Ruvu-Orkesumet wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 40.
Amefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya afya yakiwemo kujenga hospitali mpya za wilaya 67 za awamu ya kwanza, ikiwemo hospitali ya wilaya ya Simanjiro ambayo inafanya kazi na hospitali 21 za awamu ya pili na kuongeza bajeti ya afya kutoka shilingi bilioni 39 mwaka 2016 hadi zaidi ya shilingi bilioni 270 mwaka 2020 ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa dawa hadi asilimia 95, vifaa tiba na vitendanishi.