Naibu Kamanda oparesheni ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, skimu ya umwagiliaji ya kambi ya Kikosi cha 837 KJ Chita wilayani Kilombero mkoani Morogoro, Meja Mbaraka Magogo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Kamati ya Kimkakati ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) katika kikosi hicho.
Mtaalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Peter Akonaay,akielezea wanavyosaidiana na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) katika kusanifu pamoja na ujenzi.
Vijana wa JKT wakiendelea na ujenzi wa ghala la kuhifadhi mpunga lililopo katika Kikosi cha 837 KJ Chita wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro.
………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Morogoro
JESHI la kujenga Taifa JKT kupitia kikosi cha 837KJ Chita, linatarajia kuanza kujenga kiwanda kikubwa cha kuchakata zao la mpunga kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao ya mpunga yanayozalishwa kupitia kamati ya kimkakati ya kilimo, mifugo na uvuvi ya JKT ambacho kitanufaisha Jeshi hilo pamoja na Jamii inayowazunguka katika skimu hiyo.
Hayo yamebainishwa na Naibu Kamanda oparesheni ya ujenzi wa miondombinu ya umwagiliaji, skimu ya umwagiliaji ya kambi ya Chita wilayani Kilombelo mkoani Morogoro, Meja Mbaraka Magogo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya JKT katika vikosi vyake kupitia mradi huo wa kimkakati.
Meja Magogo amesema kuwa lengo la kuanzisha kiwanda hicho ni kuongeza thamani ya ubora kwenye ya mazao ya kimkakati hususani zao hilo la mpunga linalozalishwa kupitia skimu hiyo ya umwagiliaji ili kupata thamani halisi.
“Tunataka kuongeza thamani mazao yetu, pia kiwanda hiki kitaweza kuchakata mazao ya wananchi wanaoizunguka skimu hii wanapohitaji kuongeza thamani ya mazao yao,” amesema Meja Magogo.
Pia amesema wanatarajia kiwanda kidogo cha kutengeneza mitambo(work shop) ya inayotumika katika uzalishaji katika mashamba yaliyopo katika skimu hiyo ambapo pia kiwanda hicho kitatumika pia kwa wananchi wanaoizunguka skimu hiyo katika kutengeneza mitambo yao.
Amesema katika ujenzi unaoendelea katika skimu hiyo umegawanyika katika makundi mbalimbali ambapo ni miondombinu ya umwagiliaji, uandaaji wa mashamba, miundombinu ya barabara na ujenzi wa mabwawa ya Samaki na maghala ya kuhifadhia mazao mbalimbali.
Meja Magogo amesema ujenzi wa miundombinu hiyo umefanyika kwa kutumia wataalamu wa JKT, vijana askari na wataalamu kutoka tume ya taifa ya umwagiliaji ambapo tayari wameanza ujenzi wa mabanio katika mito na ujenzi wa mifereji ya kupeleka maji kwenye shamba na kutoa maji kwenye shamba.
Pia amezungumzia ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ambapo kwa sasa wameanza ujenzi wa ghala kubwa litakaloweza kuhimili mazao yote yanayolimwa hasa baada ya kuongeza zaidi uwekezaji katika kilimo tafauti na walivyoanza kilimo.
“Mwanzo wakati tunaanza shughuli za kilimo tulijenga maghala mawili yaliyokuwa na uwezo wa kubeba tani 200, lakini baada ya kuongeza uzalishaji ambapo kwa sasa tumefikia ekari 2500 ambapo tuna lengo la kufikia ekari 12000, lazima tuongeze gala kubwa litakalo himili mazao yote, ambapo mpaka sasa limetumia milioni 371 likiwa katika hatua ya lenta” amesema Meja Magogo
Kwa upande wake Mtaalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Mhandisi Peter Akonaay amesema mradi huo ulianza juni 2020, ukijumuisha hatua za usanifu na kuanza ujenzi wake.
Mhandisi Akonaay amesema baada ya kukamilika law kwa ujenzi wa mabanio sasa wameanza kujenga mifereji ya kuingiza na kutoa maji katika mashamba ambapo mifereji na 1, 2, 3, na 4 tayari imekamilika na kwamba itapelekea kuwa na kilimo ya uhakika hata mvua zikikata.