Home Mchanganyiko KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA ZATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUTOKANA NA UTABIRI WA...

KAMATI ZA USIMAMIZI WA MAAFA ZATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUTOKANA NA UTABIRI WA KIMBUNGA ‘JOBO’

0

…………………………………………………………………………………………

Kwa mujibu wa Sheria ya Menejimenti ya Maafa namba 7 ya mwaka 2015, Ofisi ya  Waziri Mkuu ina jukumu la kuratibu shughuli za maafa kwa kuhakikisha Wizara, Idara,  Taasisi, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa pamoja na asasi zote zisizo za kiserikali zinashiriki kikamilifu katika kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na kurejesha hali. 

Hivyo, Kufuatia taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini ya terehe 24 Aprili, 2021,  kuna uwezekano wa Kimbunga kutokea katika maeneo ya pwani ya nchi yetu katika  mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Tanga siku  ya Jumapili tarehe 25 Aprili, 2021. 

Imeelezwa kwamba, Kimbunga hicho kilichopewa jina la ‘Jobo’ kwa leo tarehe 24 Aprili,  2021, kipo umbali wa kilomita 200 mashariki mwa kisiwa cha Mafia. Kimbunga hicho  kimepungua nguvu kwa haraka baada ya kuingia katika mazingira yenye mzunguko wa  upepo kinzani. Hivyo, “Jobo” kwa sasa ni kimbunga hafifu kinachosafiri kwa kasi ya  kilometa 18 kwa saa baharini. Kutokana na hali hiyo, kasi ya upepo katika kitovu cha  kimbunga kwa sasa imepungua kwa kiwango kikubwa hadi kufikia kilometa 60 kwa saa.  

Aidha, kinatarajiwa kuingia nchi kavu siku ya Jumapili tarehe 25 Aprili, 2021, katika eneo  la Pwani ya Dar es Salaam na Mafia na baadae kupungua nguvu. Kwa leo kimbunga  hafifu “Jobo” kinaendelea kusogea katika eneo la pwani ya Lindi na Dar es Salaam  kikitarajiwa kuwa na kasi ya upepo wa wastani wa kilometa 40 hadi 50 kwa saa.  

Taarifa za kitaalam zinaonesha uwepo wa vipindi vya upepo mkali unaofikia kilometa 50  hadi 60 kwa saa, pia kunatarajiwa kuwepo kwa mawimbi makubwa baharini pamoja na  ongezeko la mvua kwa maeneo ya ukanda wa Pwani. Aidha, uwepo wa kimbunga ‘Jobo’

unatarajiwa kuendelea kutawala na kuathiri mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na  kusababisha ongezeko la vipindi vya mvua kwa maeneo mengine yaliyo mbali na ukanda  wa pwani (ikiwemo ukanda wa Ziwa Victoria). 

Hali hii inatarajiwa kuleta athari mbalimbli ikiwa ni pamoja na vipindi vya mvua  zinazoweza kusababisha mafuriko na upepo mkali utakaopelekea madhara ya maisha,  uharibifu wa makazi, mali, mazao mashambani, miundombinu na mazingira. Pia,  shughuli za usafirishaji kwa njia ya anga, kwenye maji na nchi kavu zitaathirika hasa kwa  mikoa husika kutokana na hali mbaya ya hewa iliyotabiriwa. 

Kufuatia utabiri huo, Ofisi ya Waziri Mkuu inatoa maelekezo kwa Kamati za Usimamizi  wa Maafa za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji katika mikoa husika nchini, ambazo ndizo  zenye jukumu kubwa la kusimamia menejimenti ya maafa, kuchukua hatua mara moja  za Kujiandaa, Kupunguza, Kukabili na Kurejesha hali endapo maafa yatatokea. 

Ili kutekeleza agizo hili kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya Mwaka 2015, ninaziagiza Kamati za Usimamizi wa maafa ziwajibike kutekeleza  mambo yafuatayo; katika mikoa ya Pwani (ikiwemo kisiwa cha Mafia), Lindi, Mtwara, na  Dar es Salaam:- 

  1. Wananchi washauriwe kuhakikisha paa za nyumba zipo imara, kupunguza matawi  ya miti iliyopo karibu na nyumba, kufunga milango na madirisha muda wote,  kuondoa vitu vinavyoweza kupeperushwa katika makazi na kuzima vifaa vyote vya  umeme na gesi. Aidha, washauriwe kuwa na akiba ya chakula cha kutosha ili  kuepuka safari zisizo za lazima. 
  2. Kamati zishirikiane na mamlaka husika kuwashauri Wananchi wasimamishe  shughuli mbalimbali zinazofanywa kandokando na ndani ya Bahari ya Hindi  hususani uvuvi, biashara ndogondogo, usafirishaji wa majini na anga katika kipindi  hicho kilichotabiriwa kuwa hatarishi ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.  
  3. Kamati ziendelee kutoa tahadhari katika mitaa mbalimbali ya mikoa hiyo juu ya  uwepo wa hali hiyo hatarishi pamoja na hatua muhimu za kuchukuliwa ili kupunguza  madhara ya kimbunga hicho endapo kitatokea. 
  4. Kamati zishirikiane na wadau wa maafa katika kufuatilia hali hii kwa ukaribu na  kujiandaa kwa pamoja katika kukabili maafa kwa kutoa misaada mbalimbali ya  kibinadamu endapo itahitajika. 

Nachukua fursa hii kutambua hatua mbalimbali ambazo zimekua zikichukuliwa na viongozi,  Kamati za Maafa na wataalamu katika sekta mbalimbali kwa kushirikiana na wanachi katika 2 

kukabiliana na Maafa. Pamoja na kazi nzuri ambayo inaendelea kufanyika, naelekeza  hatua stahiki ziendelee kuchukuliwa kuhakikisha tunakuwa na hali ya utayari ili kupunguza  madhara ya kimbunga na mafuriko yaliyotabiriwa. 

Vilevile, Wananchi wote wanaelekezwa kuchukua hatua kwa kuwa suala la kushughulikia  maafa kisheria ni la kila mmoja wetu kwa nafasi yake. Hivyo, kila mwanachi anapaswa  kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuzuia, kupunguza madhara, kukabili na kurejesha hali  endapo maafa yatatokea. 

Kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha maisha na  mali za wananchi zinakuwa salama kutokana na majanga yaliyotabiriwa. Hivyo, wananchi  wote mnaombwa kufuatilia na kuchukua hatua kutokana na taarifa na tahadhari za mara  kwa mara zinazoendelea kutolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa.