************************
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu Bi. Miriam Mmbaga ametaka suala la huduma za Afya kuwa ni mojawapo ya vipaumbele katika mkoa wa Simiyu, hasa Afya ya mama na mtoto.
Ameyasema hayo alipofanya ziara Wilayani Busega na kukutana na watumishi wa idara ya Afya. Ziara hiyo iliyofanyika tarehe 22 Aprili, 2021 wilayani Busega ililenga kujadili hali ya vifo vya akina mama na watoto, kukagua ujenzi wa miundombinu katika hospitali ya Wilaya ya Busega na kituo cha Afya Lukungu.
Mmbaga amesema suala la Afya ni muhimu sana kwa wananchi, kwani kukosekana kwa Afya iliyo bora hupunguza nguvu kazi, hivyo huathiri uchumi wa Taifa. “Ili kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto ni vyema viongozi kuacha mitazamo hasi, ambayo huathiri sekta ya Afya na kupelekea athari nyingi kwa wananchi ikiwemo vifo kwa wakina mama vinavyotokana na uzazi”, alisema Mmbaga.
Aidha, Mmbaga ametaka uwepo wa uwazi na uwajibikaji ili kuboresha huduma za Afya Wilayani Busega. “Tuwe na utamaduni wa kuwa na uwazi na uwajibikaji, ili kuleta ufanisi mkubwa katika kutekeleza majukumu yetu, ikiwemo suala la mapato na matumizi ya fedha tunazokusanya, hii itasaidia wananchi kuelewa matumizi sahihi ya fedha zinazokusanywa”, aliongeza Mmbaga.
Awali, Mganga Mkuu Wilaya ya Busega Dkt. Godfrey Mbangali, amesema baadhi ya vifo vya akina mama vinavyosababishwa na uzazi, hutokana na imani potofu katika jamii zetu. “Wengi wanatumia uzoefu wa huduma za uzazi kwa kutumia wakunga, hujifungulia nyumbani na kusababisha vifo kutokea kwani hushindwa kuwa na ujuzi zaidi kuhusu Afya ya uzazi” alisema Dkt. Mbangali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera, ametaka elimu ya Afya ya uzazi itolewe zaidi kwa wananchi ili kupunguza vifo vya akina mama. Mhe. Mwera ametaka elimu hiyo iwe ya kina ili kuleta uelewa zaidi kwa wananchi. Pia, Mhe. Mwera amewataka wahudumu wa Afya kuwa na msukumo na hali ya kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya utoaji wa huduma za Afya ulio bora Wilayani Busega.
Kwa upande mwingine, Mmbaga ametaka watumishi wa umma kupenda kazi zao kwani ni moja ya jambo muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
“Lazima kuwe na tija ya motisha katika kutekeleza majukumu ya kila siku, motisha huanza na mtumishi mwenyewe, lakini pia watumishi watambuliwe na kuthaminiwa”, aliongeza Mmbaga.
Katika ziara hiyo Mmbaga ameweza kukagua ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi katika hospitali ya Wilaya ya Busega na ujenzi wa jengo la upasuaji kituo cha afya Lukungu na kuridhishwa na ujenzi wa miundombinu hiyo.