Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) .
Afisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Nyaisa Godfrey (kushoto) akiwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) .
Baadhi ya Watendaji wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)
*******************************
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.
Waziri wa Viwanda na Biashara Profesa Kitila Mkumbo amesema kuwa Wizara yake itaendelea kutoa kutoa ushirikiano Ofisi ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili kuhakikisha inatoa huduma bora.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Prof. Mkumbo amesema kwa sasa BRELA wanapaswa kuboresha mifumo ya kutoa taarifa ili zijulikane na kila mtu anayetaka kufanya uwekezaji.
” Mnatakiwa kuhakikisha mnatoa taarifa za BRELA kwa umma ili iwe kazi nyepesi kwa mtu anayetaka kuwekeza hapa nchini au kusajili kampuni” amesema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo amesema kuwa wakati umefika kwa BRELA kupanua wigo wa kutoa huduma katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Amesema kuwa kuajiri wafanyakazi wapya inaweza kuchukua muda mrefu kwa sasa ila wanaweza kuingia mkataba na kampuni binafsi kwa kuwasaidia baadhi ya majukumu.
Amewataka watendaji wa BRELA kufata kanuni na taratibu za kazi jambo ambalo litawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa uweledi.
“Mnapaswa kuwa kama customer care katika kutoa huduma zenu kwa sababu nyinyi mnafanya kazi na wafanyabiashara na mimi uwa najishusha siwi kama bosi nikikutana na wafanyabiashara” amesema Prof. Mkumbo.
Afisa Mtendaji Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Nyaisa Godfrey, amesema kuwa watayafanyia kazi maagizo yote jambo ambalo litawasaidia kuendelea kutoa huduma bora.
Amesem kuwa asilimia kubwa wanafanya kazi na taasisi binafsi na wamekuwa wakijitaidi kutoa huduma kwa wakati ikiwemo kusajili kwa kampuni kwa muda mfupi.
“Nawatoa hofu watanzania wanaotaka kusajili kampuni waje kwani tunatumia muda mfupi kukamilisha utaratibu wote” amesema Bw. Godfrey.