Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge, wa kwanza kulia akiwakabidhi uongozi wa Kampuni ya Itracom Fertilizer LTD, cheti cha kuitambua kampuni hiyo kwa ajili ya kuja kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akizungumza mara baada ya kutoa cheti cha kuitambua kampuni ya Itracom Fertilizer LTD, kisha kutembelea eneo litakalojengwa kiwanda cha Kampuni hiyo Nala jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji hapa nchini TIC Dkt Maduhu Kazi akizungumza mara baada ya zoezi la kukabidhi cheti cha kuitambua kampuni ya Itracom Fertilizer LTD, inayokuja kuwekeza hapa nchini katika uzalishaji wa mbolea kwa ajili ya kilimo.
Afisa Masoko wa Itracom Fertilizer LTD, Bw. Nazaire Nduwimana akizungumza mara baada ya zoezi la kukabidhiwa cheti cha kuitambua kampuni ya Itracom Fertilizer LTD, inayokuja kuwekeza hapa nchini katika uzalishaji wa mbolea kwa ajili ya kilimo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge wa kwanza kutoka kushoto akiongoza jopo la viongozi na watendaji wa Serikali katika kukagua eneo litakalojengwa kiwanda cha kuzalisha mbolea, hiyo ni baada ya kampuni hiyo kukabidhiwa cheti cha kutambuliwa ili kuanza uwekezaji hapa nchini.
Wataalamu wa mipango miji Jiji la Dodoma wakiwaonyesha mchoro wa ramani ya kiwanja chenye ukubwa wa ekari 50 kilichotolewa na jiji la Dodoma kwa ajiri ya muwekezaji huo, atakayewekeza katika uzalishaji wa mbolea.
………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
Kero ya muda mrefu ya upungufu wa mbolea kwa ajili ya wakulima wa mazao mbalimbali hapa nchini iko ukingoni kumalizika mara baada ya kukamilika kwa taratibu kwa ajili ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea chenye uwezo wa kuzalisha takribani tani laki tano hadi sita kwa mwaka pindi kitakapo kamilika.
Kiwanda hicho ni mali ya kampuni ya Itracom Fertilizer Limited kutoka nchini Burundi, kitakachokuwa kikizalisha mbolea isiyokuwa na kemikali ambayo itakuwa ikizalishwa kwa kutumia mbolea ya samadi na madini ya fosiforasi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi cheti cha kuitambua kampuni hiyo kwa ajili ya kuanza taratibu za ujenzi wa kiwanda hicho Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amesema kiwanda hicho kitaleta mageuzi makubwa hapa nchini kwa kuwainua watanzania katika sekta ya kilimo na wale wafugaji.
“Kwanza tunawakaribisha sana hapa kwa kuwa ndipo mtakapo ishi, pili haya ni mageuzi makubwa mmetuambia mbolea haitakuwa na kemikali hii itasaidia hata kwa wakulima wetu mbogamboga watazalisha vyakula visivyokuwa na kemikali, pia tutalinda mazingira yetu na ardhi kwa kuwa haitaharibiwa na kemikali zinazopatikana kwenye mbolea” amesema Dkt Mahenge.
Amewahakikishia wawekezaji hao kutoka nchi jirani ya Burundi kuwa uwekezaji huo utakwenda vizuri hasa kwa kuwa wawekezaji hao walipokelewa na aliyekuwa Makamu wa Rais ambaye kwa sasa ndio Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwepo kwa kiwanda hicho kutatatua changamoto ya uhaba wa mbolea hapa nchini na pia utapunguza gharama zilizokuwa zikitumika na Serikali katika kuagiza mbolea nje ya nchi na kutumia fedha nyingi za kigeni ila sasa mbolea hiyo itazalishwa hapa nchini.
Amezitaka taasisi zote zinazohusika kutekeleza majukumu yao kikamilifu kwa manufaa ya watanzania kwani kiwanda hicho kitakapokamilika kitawanufaisha watanzania wengi kupata ajira za moja kwa moja na za mda, huku akizihimiza taasisi kuhakikisha zinafikisha huduma za kijamii katika maeneo hayo ya ujenzi ikiwa ni umeme, maji na bara bara.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji hapa nchini TIC Dkt Maduhu Kazi amesema kitendo cha Kampuni hiyo kupewa cheti cha utambuzi ni ishara kuwa imekamilisha hatua zote za kiuwekezaji na sasa wapo tayari kuanza kujenzi wa kiwanda hicho kitakachojengwa eneo lililotengwa na jiji la Dodoma kwa ajiri ya uwekezaji la Nala.
Amesema taratibu za usajili wa kampuni hiyo zilianza tangu Septemba, 2020 na mpaka sasa wamekamilisha kila kitu, huku akibainisha wamejipanga sawasawa katika kuhakikisha wanawapokea wawekezaji wengi hapa nchini.
Ameongeza kuwa “Katika taarifa tulizonazo kiwanda hiki pindi kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuajiri rasmi wafanyakazi elfu tatu(3000) na ajira zisizo rasmi zaidi ya elfu tano (5000) huku akiwa taka watakao bahatika kupata ajira hizo kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidi.
Nae Afisa Masoko wa Kampuni ya Itracom Fertilizer Limited Bw. Nazaire Nduwimana, kwa niaba ya Kampuni hiyo wameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapokea vizuri, na kusema kitendo hicho kitaendelea kudumisha undugu wa muda mrefu uliopo kati ya nchi hizo mbili za Tanzania na Burundi.
Amesema kiwanda hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani laki tano hadi sita pindi kitakapoanza kufanya uzalishaji na kitakuwa na uwezo wa kutoa ajira rasmi elfu 3000 na zisizo rasmi zaidi ya elfu 5000.
“Kiwanda hiki kikianza kuzalisha kitakuwa na manufaa kwa watanzania, kwa sababu kiwanda kitatumia madini ya fosifirasi yanapatikana kwenye minjingu, huku tutatoa ajira zaidi ya elfu moja mia tano zilizo rasmi na nyingine nyingi zisizo rasmi katika machimbo hayo ukiacha wale wafugaji wa mifugo” amesema Nazaire.