Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Idara Kuu Afya, Prof. Abel Makubi amevishauri vituo vya kutolea huduma za afya nchini pamoja na Taasisi nyingine zenye uhitaji wa barakoa kununua bidhaa hiyo kutoka Bohari ya Dawa (MSD) ili kuwa na uhakika wa ubora katika matumizi yake.
Katibu Mkuu ameyasema hayo leo alipotembelea Kiwanda cha kuzalisha Barakoa cha MSD kilichopo Keko jijini Dar es Salaam kujionea namna uzalishaji wa Barakoa unavyofanyika, ambapo pamoja na mambo mengine amefurahishwa na ubunifu wa kuanzisha na kuendesha kiwanda hicho hasa ukizingatia kuwa shughuli zote za ufungaji mtambo na uzalishaji barakoa umefanywa na wataalamu wa ndani.
Aidha, Katibu Mkuu huyo amewataka MSD kuutunza mtambo huo vizuri na kwa uangalifu mkubwa ikiwa ni pamoja kuufanyia maboresho ya mara kwa mara ili uweze kudumu kwa muda mrefu, kutoa bidhaa zenye ubora na kuonesha thamani ya fedha ya Serikali ambayo imewekezwa kwenye kiwanda hicho.
Kwa upande mwingine Prof. Makubi ameiagiza MSD kupanua wigo wa soko lake la barakoa badala ya kutegemea soko la ndani pekee ili kuwa na uwanda mkubwa wa biashara.