Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali bungeni kuhusu kigezo cha tozo ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Kilimo Tanzania, bungeni jijini Dodoma.
**************************************
Na, Saidina Msangi, WFM, Dodoma
Serikali imesema kuwa ada ya tathmini ya mikopo inayotozwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ni kwa ajili ya kulipia gharama za uchambuzi wa maombi ya mkopo ambayo ni pamoja na shajala, uhakiki wa mradi na dhamana ya mkopo.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Halima Mdee, aliyehoji kigezo cha tozo ya asilimia moja kwa mkopaji wa Benki ya Kilimo ambapo asilimia 50 inalipwa kabla ya kuanza kufanya tathmini na asilimia 50 inalipwa baada ya mkopo kuidhinishwa.
Dkt. Mwigulu amesema kuwa kigezo kinachotumika kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo ni gharama halisi za uchambuzi wa maombi hayo zinazotokana na nguvu ya soko kwa wakati husika, utaratibu huo ni wa kawaida kwa taasisi za fedha kutoza ada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo.
“Endapo mkopo hautaidhinishwa, asilimia 50 ya asilimia moja iliyolipwa hairejeshwi kwa mwombaji wa mkopo kwa kuwa kiasi hicho kimetumika kulipa gharama za uchambuzi wa mkopo”, alifafanua Dkt. Mwigulu.
Aidha alisema kuwa Sekta ya kilimo inapata mikopo kidogo kutokana na changamoto ya mikopo chechefu kama ilivyobainishwa katika ripoti ya Mdhibti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambapo kiasi cha Sh. Bilioni 129 kilirekodiwa huku Sh. bilioni 2.1 tu iliweza kurejeshwa.
Alisema kuwa Serikali inampango wa kubadilisha sekta ya kilimo kuwa ya uhakika ili kuwezesha wakulima kurejesha mikopo, matumizi ya mbegu bora, kilimo cha umwagiliaji, uhifadhi na masoko ambayo yatamuwezesha mkulima kuwa na uhakika wa kurejesha mkopo na hata benki kuwa na uhakika wa makusanyo na riba kuwa rafiki.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali itaendelea kuiangalia benki hiyo kuona namna ya kuiwezesha kimtaji ili kuwezesha kukuza uchumi wa viwanda na kukuza kipato cha wananchi kwa ujumla ili kusonga mbele kiuchumi.