TIMU ya Ulomi FC wameibuka washindi wa mashindano ya Kombe la Kichangani Bodaboda Football kupinga ukatili wa kijinsia baada ya kuifunga timu ya Kontena Bodaboda FC bao 1-0 na hivyo kuchukua zawadi ya mbuzi.
Mashindano hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki katika Uwanja wa Kunguru uliopo Goba jijini Dar es Salaam na timu zilizoshiriki ni Wagwani FC ,Ndambi Bodaboda FC,Kontena Bodaboda FC na Ulomi Bodaboda FC.
Akizungumza baada ya kukabidhi zawadi ya Mbuzi kwa bingwa wa mashindano hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Gender Action Tanzania (GATA) ambao ndio waandaji wa mashindano hayo kwa timu za waendesha bodaboda, Neema Makando amesema lengo ni kuendelea kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii na kupitia mashindano hayo yatasaidia kufikisha ujumbe kwa jamii.
Amesema kwamba kikubwa ambacho GATA wanahimiza ni jamii kuacha masuala yanayohusu ukatili wa kijinsia ambapo ameweka wazi michezo imekuwa sehemu mojawapo ya kuunganisha watu na kuleta upendo.”Katika michezo hakuna magomvi na sote tunatambua magomvi ni chanzo cha ukatili wa kijinsia na sisi hatutaki kuona ukatili wa kijinsia unaendelea kutokea.”
Makando amesema kwamba mashindano hayo ni mwanzo wa kuelekea katika ratiba ya Marathon ya kupinga ukatilii ambayo itafanyika Mei 9 mwaka huu huku akisisitiza mkakati uliopo baadae ni kuwa na timu nyingi za mpira wa miguu ambazo zitashiriki pamoja na michezo mingine,lengo kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua umuhimu wa kukomesha matukio ya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Aron Nyanda aliyekuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo amewapongeza GATA kwa kuandaa mashindano hayo kwa waendesha bodaboda kwani ni kundi kubwa na muhimu katika jamii ambalo likishirikishwa kwenye mapambano ya kupinga ukatili wa kijinsia ni rahisi kufanikiwa.
Amesema kwamba jamii ya waendesha bodaboda kwake anaiona kama taasisi rasmi na imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika jamii hasa ya kusafirisha watu pamoja na bidhaa na hivyo wamekuwa wakipita sehemu mbalimbali na iwapo wataona tukio la ukatili wa kijinsia ni rahisi kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali ya mtaa.
“Unaweza kupita sehemu ukakuta mtoto anapigwa isivyokawaida, hivyo sio lazima uchukue hatua hapo hapo lakini unaweza kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ambaye atafuatilia kujua kuna nini,”amesema Nyanda.
Katika mashindano hayo washindi wa pili ambao ni Ulomi Bodaboda FC wao wamepewa zawadi ya Vizibao vyenye kuakisi mwanga (Reflekta) ambapo Nyanda ambaye amewahi kuwa mchezaji wa zamani wa timu ya soka ya Yanga ya Dar es Salaam amesema kwenye.michezo amani na upendo hutawala na anaamini hata Mbuzi huyo supu yake itanywewa na timu zote.
Aidha amesema TFF inajisikia faraja wanapoona wadau mbalimbali wanajitokeza kuandaa mashindano ya mpira wa miguu ambapo ametumia nafasi hiyo kuzungumzia nidhamu katika michezo ni lakini akaendelea kusisitiza umuhimu wa kupinga ukatili wa kijinsia kama lengo la mashindano hayo yanavyohamasisha.
Mwakilishi kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Aaron Nyanda akikabidhi zawadi ya Vizibao vyenye kuakisi mwanga (Reflekta) kwa Kiongozi wa Timu ya Kontena FC, baada kuibuka washindi wa pili katika mashindano ya Kombe la Kichangani Bodaboda Football kupinga ukatili wa kijinsia,mashindao hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Kunguru-Goba mkoani Dar es Salaam.Pichani wa pili kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Gender Action Tanzania (GATA), Neema Makando.
Golikipa akiokoa mpira wa hatari kutoka kwa mchezaji wa timu ya Ulomi FC
Gooooo….! Timu Ulomi FC ilipojipatia goli la kwanza dhidi ya timu ya Kontena FC
Mpambano ulikuwa mkali,kila timu ilionesha uwezo wake uwanjani
Afisa Maendeleo Jamii Mbezi Juu Bi Julieth Nzugika akizungumza jambo kwa wachezaji mara baada ya mechi kuisha.