Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji
(Mstaafu) Dkt. Steven James Bwana amewataka Viongozi walioteuliwa, wanaoteuliwa
na kupewa dhamana ya Uongozi kuwa wanapaswa
kufahamu mambo ya msingi yanayohusu haki za watumishi ili wanapochukua hatua za
kinidhamu watoe uamuzi wa haki.
Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana amesema haya Jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa
Tume ya Utumishi wa Umma unaoendelea kufanyika wa kupokea, kujadili na kutolea
uamuzi rufaa na malalamiko mbalimbali ya watumishi wa umma yaliyowasilishwa
Tume.
“Tunapojadili na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko mbalimbali yaliyopo mbele yetu tunabaini
uwepo wa uzembe mkubwa unaofanywa na baadhi ya Waajiri na Mamlaka za Nidhamu wa kutokufuata Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wa kushughulikia masuala ya
nidhamu ya watumishi walio chini yao. Kuna ucheleweshaji wa kuchukua hatua kwa baadhi ya Mamlaka hizi, kutokuchukua hatua stahiki kwa wakati kunaisababishia
hasara Serikali” alisema Mheshimiwa Dkt. Bwana.
“Mtumishi wa umma anatuhumiwa kwa kosa la utoro kazini kwa zaidi ya siku tano bila ruhusa
ya Mwajiri wake. Lakini baadhi ya Wajiri au Mamlaka za Nidhamu zinachukua hatua baada ya kipindi cha zaidi ya miaka miwili. Si sawa na huu ni uzembe mkubwa. Sheria
imeelekeza hatua za kuchukua pale inapobainika mtumishi wa umma hayupo katika kituo chake cha kazi kwa zaidi ya siku tano bila ruhusa” alisema.
Jaji (Mstaafu) Dkt. Bwana alisema kuna umuhimu sana kwa Viongozi waliokwisha teuliwa na wanaoteuliwa kushika nafasi mbalimbali katika Utumishi wa Umma kupatiwa
mafunzo kuhusu Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali ili wafahamu mambo ya msingi ya kurejea wakati wa kutoa uamuzi wakati
wanaposhughulikia masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa watumishi walio chini yao” alisema.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume, Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) John Haule amesema baadhi ya Mamlaka za Nidhamu zimekuwa zinachelewa kutekeleza maagizo ya Tume bila sababu ya msingi.
“Tume kupitia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa mbele yetu tumebaini udhaifu kwa
baadhi ya Wakurugenzi na Mamlaka za Nidhamu wa kushindwa kutekeleza maagizo ya
Tume. Mamlaka za Nidhamu zitekeleze maagizo ya Tume yanayotolewa kwa mujibu wa
Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo, kama hawakuridhika na uamuzi wetu wanayo
nafasi ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais” alisema Mheshimiwa Haule.
Akizungumza katika mkutano huu Kamishna wa Tume, Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay, amesema Viongozi wanapaswa kuepuka kutenda ndivyo sivyo, wanapaswa kutenda haki kwa watumishi wanaowasimamia. Hii itapunguza malalamiko ya watumishi. Kwa watumishi wa umma, alisema wanapaswa kufahamu kuwa kutoa taarifa
za uongo kwa mwajiri ni kosa.
“Watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia utoaji wa taarifa sahihi wakati wa kujaza fomu za taarifa zao binafsi na fomu za Mfumo wa Wazi wa Mapitio na Tathmini ya Utendaji Kazi (OPRAS), wakidanganya au wakitoa zisizo taarifa sahihi watachukuliwa stahiki” alisema.
Mkutano wa Tume umeendelea leo tarehe 19 hadi 23 Aprili, 2021 ambapo rufaa na malalamiko ya watumishi wa
umma yaliyowasilishwa Tume yatatolewa uamuzi.
Imeandaliwa na:-
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
19 Aprili, 2021