
Mbunge wa Vijana Taifa, kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga akizungumza kwenye kikao cha Baraza la UVCCM, Wilayani Hanang’ ambapo alikabidhi mifuko 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilayani Hanang’, katikati ni Mwenyekiti wa UVCCM Wilayani Hanang’ Yohani Leonce na Katibu wa UVCCM Wilayani Hanang’ Raphael Ngoitek Kivuyo.

Mbunge wa Vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga akimkabidhi Mwenyekiti wa jumuiya ya UVCCM Wilaya ya Hanang’ Yohani Leonce (kushoto) moja Kati ya mifuko 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilayani Hanang’.
*****************************************
MBUNGE wa Vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga amekabidhi mifuko 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makazi ya Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilayani Hanang’.
Halamga akizungumza kwenye kikao cha Baraza la UVCCM Hanang’ kilichofanyika mji mdogo wa Katesh, amesema amejitolea mifuko hiyo ya saruji ili kuunga mkono juhudi za maendeleo ya vijana hao.
Amesema baada ya kutoa mifuko hiyo 80 ya saruji, ataendelea kushirikiana vijana wa UVCCM wilayani Hanang’ na Taifa kwa ujumla ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Ameahidi kushirikiana na vijana wa Hanang’ kuhakikisha wanapiga hatua ya maendeleo na pia wampe ushirikiano wa kutosha Mwenyekiti wao mpya wa jumuiya hiyo.
“Wajumbe mpeni ushirikiano Mwenyekiti mpya wa UVCCM Wilayani Hanang’ Yohani Leonce ili kuendelea mbele katika kuijenga jumuiya yetu kwani kuchagukiwa ni jambo moja na uongozi ni jambo lingine,” amesema Halamga.
Mbunge wa Jimbo la Hanang’ mhandisi Samwel Hhayuma amewaahidi vijana kushirikiana na pacha wake Halamga ili kufanikisha ujenzi wa nyumba hiyo ndani ya mwaka huu ikamilike.
Mhandisi Hhayuma amesema wao kama wabunge wanaotoka wilayani Hanang’ wataendelea kushirikiana ili kujenga eneo lao nao washikamane ili kuendeleza maendeleo.
“Vijana wana nguvu hivyo wawe wa kwanza kuijenga Hanang’ kwani Hanang’ itajengwa na wana Hanang’ pekee siyo watu wengine kutoka nje ya hapo,” amesema mhandisi Hhayuma.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa UVCCM Wilayani Hanang’ Yohani Leonce amemshukuru Halamga kwa kujitolea mifuko hiyo 80 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya makazi ya katibu wao.
Leonce pia amemshukuru mbunge wa jimbo hilo mhandisi Hhayuma kwa kuwaunga mkono kwenye kutimiza azma yao ya ujenzi wa nyumba ya makazi ya mtumishi wa jumuiya yao.
“Sisi vijana wa Hanang’ tutaendelea kuthamini mchango wenu wa wakati wowote katika kushirikiana kuijenga na kuilinda jumuiya yetu ya UVCCM Hanang’,” amesema Leonce.