***************************
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam.
Klabu ya Taliss –IST imenyakuwa ubingwa wa Taifa wa mashindano ya kuogelea baada ya kukusanya pointi nyingi zaidi ya klabu nyingine tano zilizoshiriki katika mashindano hayo.
Klabu hiyo imepata jumla ya pointi 1, 826 ambapo pointi 586 zilikusanywa kwa upande wa wanawake na pointi 1, 160 zilikusanywa kwa upande wa wanaume.
Huu ni ubingwa wa tatu mfululizo kwa klabu hiyo tokea mwaka 2018. Mwaka 2019 pia ilitwaa ubingwa huo na mwaka jana mashindano hayo hayakufanyika kutokana na ugonjwa wa virusi vya corona.
Meneja wa klabu hiyo Hadija Shebe alisema kuwa moyo wa kujituma, mafunzo mazuri na ushirikiano baina ya shule, klabu na wazazi ndiyo nguzo pekee ya kupata mafanikio katika mashindano hayo yaliyoshirikisha waogeleaji zaidi ya 90.
“Waogeleaji wetu wamefanya vizuri sana na wanahitaji pongezi, tunajivunia kwa mafanikio haya, ni makubwa kwa upande wa klabu hasa baada ya kuunganika na shule,” alisema Hadija.
Klabu ya Bluefins ya jijini ilishika nafasi ya pili kwa kupata pointi 1,748 baada ya kupata pointi 818 kwa upande wa wavulana na pointi 862 kwa wasichana.
Muasisi na kocha wa klabu hiyo, Rahim Alidina, aliwapongeza waogeleaji wote, makocha na wazazi kwa ushirikiano na kuifanya klabu yao kumaliza katika nafasi ya pili.
Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Klabu ya Dar es Salaam (DSC) ambayo ilipata pointi 1,486 ambapo kwa upande wa wanaume walipata pointi 888 na pointi 538 zilikuwa kwa wanawake huku nafasi ya nne ikienda kwa Mwanza kwa kupata pointi 904 na kufuatiwa na FK Blue Marlins katika nafasi ya tano kwa kupata pointi 578 na Mis Piranhas wakishika nafasi ya sita kwa kupata pointi 410.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kuogelea Tanzania (TSA), Inviolata Itatiro alisema mashindano hayo yamefanikiwa na waogeleaji kuleta ushindani mkubwa.