**********************************
TAMWA ZNZ
WAKAZI wa Shehia ya Mtambwe Kaskazini Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba wamesema vyombo vya sheria kuendelea kutoa adhabu ndogo kwa watuhumiwa wa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia ndicho chanzo cha matendo hayo kuendelea kuongezeka na kupelekea athari zaidi katika jamii.
Wameyabainisha hayo wakati wa mkutano wa kamati za kupinga udhalilishaji wilaya ya Wete wenye lengo la kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya kupinga udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo elimu ya namna ya kuibua na kufuatilia kesi hizo katika vyombo vya sheria.
Othman Haji Kibano akizungumza katika mkutano huo ulioratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) alisema licha ya juhudi zinazochukuliwa na wanajami kuripoti taarifa za matukio hayo yanapojitokeza lakini mwenendo wa hukumu na adhabu ndogo kwa watuhumiwa zinawakatisha tamaa na kusababisha wadhalilishaji kuendelea na vitendo hivyo bila hofu yoyote.
“Wanajamii tunajitahidi sana kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za vitendo hivi lakini tukimpeleka mtuhumiwa leo Polisi cha kushangaza baada ya siku tatu tunamuona amerudishwa mtaani. Hii inatuvunja sana moyo kwani sisi ndio tunaoumia huku mtaani,” alisema.
Naye Hamad Idd Hamad alisema, “kama kweli serikali inataka vitendo hivi vimalizike katika jamii basi wasiwaachilie huru watuhumiwa hawa kwa adhabu ndogo kwani kunawafanya hawajutii na matokeo yake wanarudia na kuendelea kuharibu watoto wetu.”
Aliongeza kuwa kutokana na mwenendo wa watuhumiwa kuachiwa huru hupelekea baadhi yao kukata tamaa ya kuripoti kesi hizo jambo ambalo linahatarisha zaidi usalama wa watoto.
Mapema afisa ustawi wa jamii Wilaya ya Wete, Haroub Suleiman Hemed alisema jamii haipaswi kukata tamaa juu ya utoaji taarifa za matendo hayo kwani kufanya hivyo kutazidi kuwapa nguvu wadhalilishaji kuendelea kuharibu watoto bila hofu yoyote.
“Watu wengi wanadhani kwamba njia sahihi baada ya kutokea tukio la udhalilishaji ni kukaa na kumaliza nyumbani, hawaangalii madhara yanayompata mwathirika. Nikuombeni tuache tabia hizi kwani kufanya hivyo tunawaweka watoto wetu katika hatari zaidi ya kufanyiwa udhalilishaji,” alisema.
Mkuu wa upelelezi na mratibu wa dawati la kijinsia kutoka Jeshi la Polisi Wete, Fakih Yusuf Mohd amewataka wanajamii kutoa mashirikiano ya taarifa pale linapotokezea tukio ili uchunguzi uweze kufanyika kwa wakati na mtuhumiwa achukuliwe hatua kisheria.
“Tunafahamu kuna baadhi ya akari si waadirifu sana, lakini nakuombeni, ukimwona askari polisi anakushawishi upatane na mdhalilishaji ili kuimaliza kesi kataa. Sisi jeshi la polisi tunahitaji taarifa kutoka kwenu ili tufanye kazi yetu. Hii kazi haihitaji muhali kufanikiwa kwake,” alisema.
Juma Musa Omar kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Wete alisema serikali kupitia ofisi hiyo imeweka mkakati maalum wa kuzisimamia kesi za udhalilishaji ili kuhakikisha zinapata hukumu na watuhumiwa wanatumikia adhabu kwa mjibu wa sheria.
“Sisi DPP tuna mkakati maalumu tunaokwenda nao. Sasa hatufuti kesi hata moja ya udhalilishaji kwa mtu anayekuja kutaka tuifute kesi hiyo, au anayegoma kuja mahakamani kutoa ushahidi, kwani tumegundua wengi wanatumia mwanya huo wa kutokwenda kutoa ushahidi ili muda ukifika kesi yao ifutwe”
Awali mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa Said alisema mkutano huo ni mwendelezo wa juhudi za TAMWA ZNZ kuisaidia serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na vitendo vya udhalilishaji katika jamii kwa kuwawezesha elimu ya ufuatiliaji na utoaji wa ushahidi mahakamani ili kujenga jamii yenye kuzingatia usawa na usalama wa kila mmoja.