Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akizungumza wakati wa uwasiloshaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ya Sekta ya Mifugo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29, 2021 bungeni Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiwa na Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul pamoja na watumishi wa wizara hiyo ya Mifugo wakati wa uwasilishaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya mwaka 2021/2022 ya Sekta ya Mifugo kwa kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo, mifugo na maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel, akiwasilisha Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2021/22 ya Sekta ya Mifugo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji iliyokutana leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Christopher Ole Sendeka, akiwaslisha hoja wakati wa uwasilishwaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Kipindi cha Mwaka 2020/21 na Makadirio ya Bajeti ijayo ya 2021/22 ya Sekta ya Mifugo leo Machi 29,2021 bungeni Dodoma.
…………………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.Mashimba Ndaki,amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2021/22 wamepanga kuboresha sekta ya mifungo kwa kujenga majosho 129, ili kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na mazao ya mifugo.
Mhe.Ndaki ameyasema hayo bungeni Dodoma wakati wizara yake ilipokuwa ikiwasilisha bajeti ya sekta ya mifugo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji.
Waziri Ndaki amesema kuwa Wizara yake imedhamilia kufanya maboresho makubwa katika sekta ya mifugo ili kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na mifugo na kuchangia pato la taifa.
Amesema kuwa eneo ambalo watalifanyia kazi ni kujenga majosho 129, mapya pamoja na kukarabati yaliyopo ili kusaidia wafugaji kupata huduma hizo katika maeneo yao,
“Tutahakikisha kuwa tunajenga majosho kwa ajili ya kuogeshea mifugo kila eneo lenye mifugo nchini lakini pia kukarabati majosho yote yalipo ili kuwezesha wafugaji kupata huduma za ugani katika maeneo yao”amesema
Mhe.Ndaki alitaja eneo jingine ambalo watalifanyia kazi ni kuboresha eneo la malisho kwa ajili ya mifugo ili kuwa na malisho ya uhakika na kupunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
“Katika hili hivi sasa tumepunguza bei ya kukodisha maeneo ya malisho kwa kukodisha kwa Sh. 3,500 kwa heka kwa mfugaji atakaye hitaji eneo la malisho”amesisitiza
Hata hivyo amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha wamepanga kukusanya mapato katika sekta kiasi cha Sh. bilioni 50.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia sekta ya mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel,akiwasilisha bajeti ya sekta ya mifugo mbele ya katimati hiyo, amesema kuwa itasaidia kuongeza thamani ya mifugo.
Prof.Gabriel amesema kuwa katika mipango ya bajeti ijayo wamepanga kuhakikisha kuwa wanawekeza katika kuboresha afya ya mifugo,pamoja na kutafuta masoko ya mazao ya mifugo.
“Katika kipindi hichi tutahakikisha kuwa tunatafuta masoko katika bidhaa za mazao ya mifugo kama vile nyama, ngozi , maziwa lakini pia kuongeza fursa nyingine ya matumizi ya vitu kama kwato, pembe na manyoya”alisema
Hata hivyo amesema kuwa mpaka sasa wameshapata wawekezaji kutoka nchi ya Slovakia, ambao wameahidi kuja nchini kuwekeza kiwanda cha kutengeneza mbolea kwa kutumia manyoya, pembe pamoja na kwato.
Aidha ametoa wito kwa wafugaji nchini kutumia fursa ya mitamba ya kisasa iliyopo katika Ranchi za taifa kufanya uhimilishaji ili kupata mifugo iliyobora ili iweze kuwainua kiuchumi na kuongeza pato la taifa.