Home Mchanganyiko Yatima wasema Rais Samia ni  chaguo la Mungu

Yatima wasema Rais Samia ni  chaguo la Mungu

0

MENEJA wa Kampuni ya Lucky Well ya China, Feng Hun Chen,akikabidhi msaada wa chakula kwa Kituo cha kulelea Yatima cha Umra, Magomeni,Dar es Salaam, kwaajili ya kuwafariji katika kipindi cha maombolezo ya msiba wa Hayati Rais Dk. John Magufuli.

*****************************

YATIMA  wamefanya dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais,  Hayati Dk. John Magufuli na kumuelezea  Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni  chaguo la Mungu.

Wamefanya dua hiyo,  katika Kituo cha Kulea Yatima cha Umra, Magomeni, leo  dua iliyoenda sambamba na upokeaji wa misaada mbalimbali kutoka  kwa kampuni ya Luckwell ya China, misaada iliyolenga kuwafariji katika kipindi cha maombolezo.

Akiongoza dua hiyo, Mwasisi wa Vituo vya  Umra, Rahma Juma, alisema,   siku ambayo  Rais samia alikula kiapo  ndiyo siku aliyokata mbeleko  ya kuwabeba watanzania hususan wanyonge na yatima.

“Cheo hicho kachaguliwa na Mungu.Hakuchaguliwa na mtu. Huwezi kumchagua   mtu kabla Mungu hajamchagua,”alisema Rahma.

Mtoto Abdulhakim Mohammed, alisema  wanamuombea Rais Samia Mungu ampe nguvu ya kufanyaa kazi kama ilivyo kuwa  kwa Hayati Rais Dk. Magufuli.

“Tunaimani Rais Samia atatusaidia hivyo hivyo. Tunamuomba Mungu  amuondolee balaa, maradhi ya kila aina na atukumbuke yatima,”alisema.

Mtoto, Yasira Dauda, alisema,  Samia kuongoza  taifa ni siri ya Mwenyezi Mungu.

“Tunaomba asichoke kutubeba,”alieleza  mtoto huyo.

Akikabidhi misaa kwa watoto hao, Meneja wa  Kampuni ya Lucky Well Feng  Hun Chen,  ambaye ni raia wa China, alimuelezea Hayati Rais Dk. J Magufuli  kuwa  aligusa maisha ya wanyonge wakiwemo watoto na kwamba ili kumuenzi ni wajibu jamii kutoa kwaajili ya makundi yenye mahitaji maalumu.

 “Tumekabidhi msaada huu wakati wa siku ya maziko ya Hayati Dk. Magufuli ili kuwafariji  yatima kwa sababu marehemu aliwathamini na  kuwajali watu wenye mahitaji maalumu kama hawa,”alisema Chen.

Alisema, msaada huo unaohusisha mchele tani moja , sukari, mafuta ya kupikia, sabuni ya unga na miche ni kwaajili ya watoto katika kipindi cha maombolezo na kuahidi kuwa wataendelea kusaidia jamii ili  kumuenzi  Hayati Dk. Magufuli.

Mfadhili wa kituo hicho cha Umra cheye watoto 117, Juma Gurumo, alisema, msiba wa Dk. Magufuli ni mkubwa  hivyo waliona kuna wajibu wa kuchangia kwa kuwapa  yatima  mahitaji muhimu hasa ya  chakula.

“ Tunaamini Hayati Rais Dk. Magufuli aliwajali wanyonge na wenye mahitaji, hivyo  wakati tukiomboleza  tumuenzi kwa kukumbuka kundi hili,”alisema Gurumo.