Home Mchanganyiko DC CHAULA ATAKA HAYATI MAGUFULI AENZIWE KWA KUTETEA WANYONGE

DC CHAULA ATAKA HAYATI MAGUFULI AENZIWE KWA KUTETEA WANYONGE

0
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoani Manyara MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau akizungumza kwenye sala na dua ya kumuombea apumzike kwa amani Rais wa awamu ya tano hayati Dokta John Magufuli.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula, akizungumza kwenye sala na dua ya kumuombea apumzike kwa amani Rais wa awamu ya tano hayati Dokta John Magufuli, katika maombolezo yaliyofanyika nje ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.

*****************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zephania Chaula amesema wanyonge wanapaswa kuendelea kutetewa ili kuenzi mema yote aliyokuwa anayafanya Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli.
Mhandisi Chaula ameyasema hayo kwenye dua na sala ya kumuombea mapumziko mema hayati Magufuli iliyofanyika kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mji mdogo wa Mirerani.
Amesema enzi za uhai wake hayati Magufuli alikuwa muumini wa kutetea wanyonge hivyo viongozi na wananchi wa Simanjiro wanapaswa kuyaenzi hayo ili kuacha kumbukumbu nzuri.
Amesema wakati wa utawala wa miaka sita wa hayati Dokta Magufuli alifika Wilayani Simanjiro mara mbili hivyo alikuwa anaipenda Wilaya hiyo ndiyo sababu akafika mara mbili kuwatembelea.
“Kuna Wilaya nyingine hazijapata bahati ya hata mara moja ya kutembelewa na hayati Dokta Magufuli ila sisi Simanjiro tumefanikiwa mara mbili tunashukuru sana,” amesema
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya mhandisi Chaula amesema ili kuenzi maendeleo yaliyofanywa na hayati Dokta Magufuli inatakiwa pajengwe mnara wa kumbukumbu na kuwekwa picha yake.
Ametaja baadhi ya maendeleo yaliyofanyika Simanjiro kipindi cha uongozi wa hayati Dokta Magufuli ni barabara ya lami ya kutoka Kia hadi Mirerani, mradi wa maji wa mto Ruvu hadi Orkesumet na hospital ya wilaya hiyo.
Ametaja miradi mingine ni ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite, chuo cha ufundi Veta cha Emboreet, shule mbili za kidato cha sita na nyingine ya tatu imepata usajili hivi karibuni.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro,Yefred Myenzi amesema hayati Magufuli amepewa majina mengi ikiwemo jiwe, chuma na jeshi kutokana na namna alivyowajali wanyonge.
“Wakati wengine wapo Chato mkoani Geita wakiaga mwili na pia wengine Dares salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Geita walikimbia kwa miguu, sisi tupo hapa Mirerani tukiomboleza kwa sala na dua,” amesema Myenzi.
Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Robert Matheus amesema hayati Magufuli aliwajali watu wenye ulemavu ndiyo sababu akaagiza wapatiwe asilimia mbili ya mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri ya wilaya.