MENEJA wa Kampuni ya Lucky Well ya China, Feng Hun Chen,akikabidhi msaada wa chakula kwa Kituo cha kulelea Yatima cha Umra, Magomeni,Dar es Salaam, kwaajili ya kuwafariji katika kipindi cha maombolezo ya msiba wa Hayati Rais Dk. John Magufuli.
*****************************
YATIMA wamefanya dua maalum ya kumuombea aliyekuwa Rais, Hayati Dk. John Magufuli na kumuelezea Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni chaguo la Mungu.
Wamefanya dua hiyo, katika Kituo cha Kulea Yatima cha Umra, Magomeni, leo dua iliyoenda sambamba na upokeaji wa misaada mbalimbali kutoka kwa kampuni ya Luckwell ya China, misaada iliyolenga kuwafariji katika kipindi cha maombolezo.
Akiongoza dua hiyo, Mwasisi wa Vituo vya Umra, Rahma Juma, alisema, siku ambayo Rais samia alikula kiapo ndiyo siku aliyokata mbeleko ya kuwabeba watanzania hususan wanyonge na yatima.
“Cheo hicho kachaguliwa na Mungu.Hakuchaguliwa na mtu. Huwezi kumchagua mtu kabla Mungu hajamchagua,”alisema Rahma.
Mtoto Abdulhakim Mohammed, alisema wanamuombea Rais Samia Mungu ampe nguvu ya kufanyaa kazi kama ilivyo kuwa kwa Hayati Rais Dk. Magufuli.
“Tunaimani Rais Samia atatusaidia hivyo hivyo. Tunamuomba Mungu amuondolee balaa, maradhi ya kila aina na atukumbuke yatima,”alisema.
Mtoto, Yasira Dauda, alisema, Samia kuongoza taifa ni siri ya Mwenyezi Mungu.
“Tunaomba asichoke kutubeba,”alieleza mtoto huyo.
Akikabidhi misaa kwa watoto hao, Meneja wa Kampuni ya Lucky Well Feng Hun Chen, ambaye ni raia wa China, alimuelezea Hayati Rais Dk. J Magufuli kuwa aligusa maisha ya wanyonge wakiwemo watoto na kwamba ili kumuenzi ni wajibu jamii kutoa kwaajili ya makundi yenye mahitaji maalumu.
“Tumekabidhi msaada huu wakati wa siku ya maziko ya Hayati Dk. Magufuli ili kuwafariji yatima kwa sababu marehemu aliwathamini na kuwajali watu wenye mahitaji maalumu kama hawa,”alisema Chen.
Alisema, msaada huo unaohusisha mchele tani moja , sukari, mafuta ya kupikia, sabuni ya unga na miche ni kwaajili ya watoto katika kipindi cha maombolezo na kuahidi kuwa wataendelea kusaidia jamii ili kumuenzi Hayati Dk. Magufuli.
Mfadhili wa kituo hicho cha Umra cheye watoto 117, Juma Gurumo, alisema, msiba wa Dk. Magufuli ni mkubwa hivyo waliona kuna wajibu wa kuchangia kwa kuwapa yatima mahitaji muhimu hasa ya chakula.
“ Tunaamini Hayati Rais Dk. Magufuli aliwajali wanyonge na wenye mahitaji, hivyo wakati tukiomboleza tumuenzi kwa kukumbuka kundi hili,”alisema Gurumo.