Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza Machi 24, 2021.
Mwili wa hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ukiwasili kwenye uwanja wa ndege wa Mwanza, Machi 24, 2021.
Msafara wa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ukipita katika barabara ya Airport kuelekea katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa ajili ya shughuli za kuagwa na maelfu ya Wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani leo tarehe 24 Machi 2021.
Msafara wa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ukiwasili katika uwanja wa CCM Kirumba kwa ajili ya shughuli za kuagwa na maelfu ya Wananchi wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani leo tarehe 24 Machi 2021.
Makamanda wa JWTZ wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli mara baada ya kuwasili ndani ya uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza. PICHA NA IKULU
…………………………………………………………………………………………..
NA BALTAZAR MASHAKA, Mwanza
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo Machi 24,2021 amewaongoza viongozi mbalimbali wa serikali katika mapokezi ya mwili wa Hayati Rais John Magufuli, ulipowsili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwanza, ukitokea Zanzibar.
Mwili huo uliwasili majira ya saa 1:31 asubuhi kwa ndege na kuondolewa uwanjani kwa gari maalum hapo majira ya saa 2:08 kuelekea kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ambako shughuli ya kuagwa na kutoa heshima za mwisho kwa kiongozi huyo ilifanyika ambapo kabl mwili huo ulishushwa na maofisa wa jeshi wenye vyeo vya Kanali n kuuingiza kwenye gari majira ya saa 2:03.
Wakati wa mapokezi hayo ya mwili wa Rais Magufuli,mbali na Waziri Mkuu, alikuwepo Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Hemed Seleman Abdallah,Waziri wa Mambo ya Nje, Ushikiano wa Afrika wa Mashariki Kikanda na Kimataifa, Profesa Paramagamba Kabudi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mali za CCM, Christopher Gachuma.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella akiambatana na Wakuu wa Mikoa ya Mara,Adam Malima,Zainabu Terack wa Shinyanga na Brigedia Jenerali,Michael Gaguti wa Kagera na viongozi wengi wa Chama na Serikali.
Mara baada ya mwili huo kuondolewa uwanjani wa ndege,vilio vilisikika kutoka kwa akina mama waliojitokeza kuupokea wakiwa wamejipanga kando ya barabara ya Makongoro kutoka uwanja wa Ndege kuelekea CCM Kirumba.
Gari lililobeba jeneza la mwili wa Rais Magufuli, ulisindikizwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi ambao waliungana na wananchi kuusindikiza kwa kukikimbia pembeni mwa gari hilo.
Msafara huo ulipita maeneo ya Ilemela, Sabasaba, Iloganzala, Pasiansi,Nyamanoro, Seleman Nassoro ambako aliwahi kuishi akiwa Waziri wa Ujenzi, Kona ya Bwiru,Gana kupitia barabara ya Furahisha hadi CCM Kirumba.
Wakati wote kwenye maeneo mwili huo ulikopita,wananchi walijipanga kando ya barabara huku wengi wakiangua vilio mara baada ya kuona msafara wa magari likiwemo lililobeba jeneza la mwili wake ambako eneo la Seleman Nassoro msafara huo ulisimama kwa dakika moja ili kutoa fursa kwa majirani zake kutoa heshima za mwisho.
Wananchi hasa akina mama walitandika khanga barabarani kuonyesha heshima kwa mwili wa Rais Magufuli, huku vijana wakiimba Magufuli Jeshi,Jeshi,Magufuli Jeshi huku wengine wakiwa wanapunga matawi ya miti baadhi wakiwa wamejipanga kando mwa barabara maeneo yote mwili huo ulikopita.
Aidha msafara huo kutoka uwanja wa ndege ulisindikizwa na chopa za JWTZ na polisi, kuhakikisha hali ya usalama inaimarishwa huku Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kallli akitembea kwa na kukimbia kutoka uwanja wa ndege muda wote akiwa pembeni mwa gari lililoubeba mwili wa Hayati Rais Magufuli.
Alionyesha kuwa Rais aliyependwa na wananchi wake, laiti leo angekuwa hai akaona jinsi Watanzania walivyojitokeza kuuaga mwili wake baada ya kifo angefarijika huko kaburini.